• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:15 PM
Wanaharakati wataka serikali ipige marufuku kemikali hatari katika dawa za kuangamiza wadudu

Wanaharakati wataka serikali ipige marufuku kemikali hatari katika dawa za kuangamiza wadudu

Na MAGDALENE WANJA

WANAHARAKATI wameitaka serikali kupiga marufuku matumizi ya kemikali hatari zinazopatikana katika baadhi ya dawa za kuangamiza wadudu waharibifu wa mimea shambani.

Wanaharakati hao walizungumza siku ya Jumatano wakati ulimwengu uliadhimisha Siku ya Chakula Duniani.

“Swala la kuwepo kwa chakula cha kutosha nchini limekuwa nyeti sana na linahuzunisha watumiaji wa vyakula hivyo. Hii ni ukiukaji wa haki za Wakenya ya kupata chakula salama,” alisema Bi Claire Nasike wa kutoka shirika la Greenpeace Africa.

Akaongeza: “Wafanyabiashara wasiowajali wananchi wanaendeelea kuongeza hatari katika chakula huku afya ikiendelea kuzorota.”

Wanaharakati sasa wameitaka serikali kupiga marufuku matumizi ya kemikali ambazo zinahatarisha maisha ilhali zinaendelea kuuzwa.

Shirika la Route to Food Initiative pia lilitoa ripoti inayoonyesha jinsi matumizi ya kemikali hizo yalivyochangia katika uchafuzi wa mchanga na chemchemi za maji ambazo zimechangia katika uharibifu wa chakula.

“Baadhi ya kemikali hizi zimeidhinishwa na Bodi ya Kudhibiti Wadudu Waharibifu – Pest Control Products Board – zina madini hatari sana kama vile Carbendazim, Carbofuran, atrazine, acephate, na permethrin ambazo zina madhara kwa wanyama wa nchi kavu na majini,” ilisema ripoti hiyo.

Wanaharakati hao sasa wameitaka Wizara ya Kilimo kuweka sheria kali zitakazolinda wananchi kutokana na wafanyabiashara.

You can share this post!

Mahujaji 35 wafa katika ajali Medina

Maji ya mafuriko kutoka Ethiopia yaitikisa Lamu

adminleo