• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
JAMVI: Raila njiapanda huku wandani na wafuasi wakitilia shaka mkataba

JAMVI: Raila njiapanda huku wandani na wafuasi wakitilia shaka mkataba

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga amejipata pabaya baada ya wandani na wafuasi wake kuanza kutilia shaka mkataba wa maelewano kuhusu ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni baada ya serikali kukataa kumruhusu wakili Miguna Miguna kurejea nchini na badala yake kumzuilia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa zaidi ya saa 48 na kisha kumfurusha kwa nguvu hadi mjini Dubai.

Kuruhusu Dkt Miguna kurejea nchini bila kuhangaishwa ni miongoni mwa masuala yaliyoko katika mkataba wa maelewno baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Alipokuwa akizungumza mtaani Kondele, Kisumu, wiki mbili zilizopita Bw Odinga aliambia wafuasi wake kuwa alihakikishiwa na Rais Kenyatta kuwa Dkt Miguna angerejea nchini bila kuhangaishwa na serikali.

Kiongozi huyo wa Upinzani pia alisema waliafikiana na Rais Kenyatta wanasiasa wote waliokamatwa au kushtakiwa kuhusiana na kuapishwa kwake kuwa ‘Rais wa Wananchi’ mnamo Januari 30, mwaka huu, uwanjani Uhuru Park waachiliwe huru na mashtaka dhidi yao yaondolewe mahakamani.

Kuanzishwa kwa mchakato wa kufanya mageuzi katika mfumo wa uchaguzi pia ni miongoni mwa masuala ambayo viongozi hao wawili waliafikiana.

Dkt Miguna alisafirishwa kwa mara ya kwanza na serikali hadi nchini Canada kutokana na madai kwamba hakuwa Mkenya. Wakili Miguna pia alishtumiwa na serikali kwa kumwapisha Bw Odinga kinyume cha sheria.

Alirejea nchini Jumatatu iliyopita lakini akazuiliwa chooni katika uwanja wa JKIA ambapo alidai kuwa alidungwa dawa ya usingizi na polisi na kutupwa ndani ya ndege hadi Dubai.

Bw Odinga amekuwa akizuru maeneo ambayo ni ngome zake kisiasa huku akiwahimiza wafuasi wake kuunga mkono mkataba wa maelewano kati yake na Rais Kenyatta.

Kiongozi huyo wa ODM pamoja na Rais Kenyatta walifaa kuanza ziara ya kuhubiri amani nchini wiki iliyopita, lakini mpango huo ukaahirishwa kutokana na ripoti za kijasusi kwamba uwanja ulikuwa telezi hasa katika maeneo anayodhibiti kisiasa kinara huyo wa upinzani.

 

Hakuna ripoti

Rais Kenyatta aliteua Balozi Martin Kimani huku Raila akimtwika Wakili Paul Mwangi jukumu la kuhakikisha wanaandaa mipango ya kuhakikisha kuwa mkataba huo unatekelezwa. Lakini kufikia sasa, wawili hao hawajatoa ripoti yoyote kuhusiana na maendeleo ya mpango huo.

Wiki iliyopita, Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale alisema Jubilee hawako tayari kufanya mageuzi katika mfumo wa uchaguzi au kubuni nyadhifa zaidi serikalini zitakazotwaliwa na Bw Odinga na wandani wake.

Kauli hiyo ya Bw Duale imesababisha wandani wa Bw Odinga kuanza kutilia shaka mkataba wa ushirikiano baina yake na Rais Kenyatta.
Jumatano, Seneta wa Siaya alipuuzilia mbali mkataba huo akisema Rais Kenyatta amewasaliti.

Bw Orengo alitoa kauli hiyo baada yake pamoja na mawakili wenzake; Julie Soweto, Nelson Havi na Cliff Ombeta kupigwa na polisi uwanjani JKIA Jumatano usiku walipokuwa wakiwapelekea stakabadhi za amri ya mahakama ya kutaka Dkt Miguna awasilishwe kortini Alhamisi asubuhi.

“Mkataba wa maelewano baina ya Bw Odinga na Rais Kenyatta ni bure, hausaidii kwa lolote,” Bw Orengo aliyekuwa amejawa na ghadhabu akaambia wanahabari.

Kiongozi wa Wachache Bungeni  John Mbadi pia amekosoa mkataba huo lakini akasisitiza kuwa bado chama cha ODM kinaunga mkono ushirikiano wao na Jubilee.

 

Kubadili nia

Alhamisi, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, alitangaza kutoa msimamo wa chama hicho kuhusiana na mkataba wa maelewano baina ya Bw Odinga na Rais Uhuru lakini baadaye akabadili nia na kuzungumzia suala la baadhi ya maafisa wa serikali kupuuza maagizo ya mahakama.

Bw Sifuna alikwepa kuzungumzia suala hilo baada ya kukutana na Bw Odinga nje ya majengo ya Mahakama ya Milimani. Bw Odinga amesalia kimya licha ya Dkt Miguna kuendelea kunyanyaswa na serikali.

Jumatatu usiku, juhudi za Bw Odinga kumwokoa Dkt Miguna uwanjani JKIA ziligonga mwamba. Bw Odinga alionekana akipiga simu mara kwa mara lakini dakika chache baadaye maafisa wa polisi walitokea na kumnyanyua Dkt Miguna hadi katika ndege ya kuelekea Dubai. Dkt Miguna alipiga kelele na kushuka kwa nguvu ambapo alizuiliwa chooni kwa zaidi ya saa 24.

Kulingana na mshauri wa Bw Odinga, Salim Lone, serikali imemsaliti kiongozi wa Upinzani kwa kuendelea kumnyanyasa  Dkt Miguna.

“Bw Odinga aliweka kando masilahi yake ya kibinafsi na kukubali kuunga mkono Rais Kenyatta. Lakini hatua ya serikali kunyanyasa Dkt  Miguna na kukiuka haki za kibinadamu ni usaliti kwa Bw Odinga,” anasema Bw Lone.

Baraza la Wazee la Jamii ya Waluo pia limeelezea wasiwasi kuwa kunyanyaswa kwa Dkt Miguna kunatishia kusambaratisha mkataba wa maelewano baina ya Bw Odinga na Rais Kenyatta.

You can share this post!

JAMVI: Huenda ushirikiano mpya wa Raila na Uhuru ukamfaa...

Kalameni atwangwa kama nyoka kufumaniwa na kisura wa sponsa

adminleo