• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
AKILIMALI: Kilimo cha ndizi ni chenye manufaa tele

AKILIMALI: Kilimo cha ndizi ni chenye manufaa tele

Na SAMMY WAWERU

KATIKA shamba la Lucy Muriithi, tunakaribishwa na rangi ya kijani cha migomba. Kuna inayozalisha ndizi, mingine inachana maua na mingine ingali midogo.

Mama huyu anatazama kifungu cha ndizi kilichoning’inia mgombani, pengine kukagua ikiwa kimetosha kuvunwa.

“Baada ya wiki kadhaa kutoka sasa nitavuna ndizi zilizokomaa,” anadokeza Bi Muriithi.

Kijiji cha Karii, Kangai Kaunti ya Kirinyaga anakokuza ndizi, shughuli mbalimbali za biashara na kilimo zimeshika kasi, angaa kujizimbulia riziki.

Wakazi waliojituma wanaonekana kujishughulisha katika kilimo cha nyanya, mboga za aina mbalimbali, mahindi, matunda na maharagwe.

Katika ekari moja ya Lucy, ameipamba kwa matunda aina ya ndizi.

Alianza kilimo cha matunda haya 2014 baada ya kuchoshwa na maharagwe ya Kifaransa maarufu kama French beans, na miaka mitano baadaye hajutii kamwe mkondo aliochukua.

“Soko la maharagwe hayo lilidorora, nikakosa kampuni za kuuzia kwa sababu yanakuzwa kupitia kandarasi. Yaliishia kuharibikia shambani,” aeleza.

Mbali na kukumbwa na masaibu tele kupata soko, anasema gharama ya kukuza French beans ni ya juu mno. Hata hivyo, moyo wa Lucy sasa unatabasamu kwani umetulizwa na kilimo cha ndizi.

Zaraa ya ndizi haina mkuno wa nywele wala akili, kwani gharama ya leba, pembejeo na mtaji ni nafuu ikilinganishwa na mimea mingine. Isitoshe, soko la mazao si kikwazo kwa sababu matunda haya yana walaji wengi. Ndizi ni zao la nne bora duniani baada ya mchele, ngano na mahindi.

Mkulima Lucy Muriithi hupanda ndizi za migomba iliyoimarishwa kitaalamu, almaarufu ‘tissue culture bananas’.

“Nilianza na robo ekari na ilinigharimu Sh25, 000 pekee,” anafichua.

Mkulima huyu anasema kilimo cha ndizi hakihitaji mwalimu. Shamba likilimwa, mashimo yenye kimo cha urefu wa futi mbili yanaandaliwa. “Shimo linapaswa kuwa na kipenyo cha futi tatu, na nafasi ya mita tatu kwa tatu mraba – kutoka shimo moja hadi nyingine,” akaelezea.

Yanawekwa mbolea, karibu mageleni au madoo mawili kila shimo na mkulima huyo huichanganya na fatalaiza yenye madini ya Ammonia, Phosphorous na Nitrogen. Pia, hutia dawa dhidi ya wadudu.

“Nikishapanda, hurejesha udongo hadi kimo cha futi moja. Nafasi iliyosalia ni ya kutunza migomba kwa maji na mbolea,” asema. Ekari moja inasitiri takriban mbegu 1, 600 moja ikigharimu kati ya Sh70 – 100.

Bw James Macharia, mtaalamu, anasema ili kupata mazao bora, mengi na ya kuridhisha, machipukizi yanayotoka kandokando mwa mgomba mama uliopandwa yanapaswa kupogolewa na kusalia na manne pekee.

“Machipukizi mengi huleta ushindani wa lishe; maji na mbolea. Ni heri kusalia na machache yatakayotoa mazao ya kuridhisha,” anasema Bw Macharia.

Baadhi ya wakulima wangali wanaendelea kukuza ndizi kupitia mfumo wa zamani, ambapo machipukizi yanayojitokeza kandokando mwa migomba mama hutolewa na kutumika kama mbegu. Inatumika kwa msingi kuwa inapunguza gharama, pamoja na kupandwa moja kwa moja.

Akiwahimiza kukumbatia tissue culture bananas, Bw Macharia anasema mfumo wa zamani una changamoto zake kwani migomba na mazao huathiriwa upesi na wadudu na magonjwa kama Fusarium wilt, Sigatoka na Bacterial wilt.

Magonjwa ya virusi kama banana streak na bunchy top, yanasambazwa na machipukizi hayo. Fukusi na Nematodes, ni wadudu wanaoshuhudiwa mara kwa mara kwa migomba iliyopandwa kutoka kwa machipukizi. Mbali na kuwa na mazao duni, mtaalamu huyu anasema mfumo wa zamani unachukua muda mrefu kuzalisha.

“Ndizi zilizoimarishwa kitaalamu zinakidhi vigezo vya uhitaji wa soko pamoja na kusaidia kuongeza mapato kwa wakulima, wafanyabiashara husika na kunufaisha taifa kwa jumla,” anafafanua.

Ekari moja iliyotunzwa vyema ina uwezo kuzalisha zaidi ya tani 25, sawa na kilo 25, 000.

Hapa nchini ndizi hununuliwa kwa vifungu, na kulingana na Lucy Muriithi kimoja ni kati ya Sh400 – 800. Wateja wake hutoka Kagio na wengine masoko ya Nairobi.

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Sanaa inafanya avume ugenini

FUNGUKA: ‘Nimemweka mahali pema moyoni…’

adminleo