• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
FUNGUKA: ‘Nimemweka mahali pema moyoni…’

FUNGUKA: ‘Nimemweka mahali pema moyoni…’

Na PAULINE ONGAJI

KUNA msemo kwamba kifo ni sawa na kikohozi na kikifika, basi hakiwezi epukika.

Na nina uhakika kwamba Betty ni miongoni mwa watu wanaokubaliana na kauli hii.

Binti huyu alimpoteza mchumbake miaka mitatu iliyopita baada ya mwanamume huyo kuugua kwa muda mfupi.

Betty mwenye umri wa miaka 36 ni afisa wa masuala ya kifedha katika kampuni moja.

Miaka mitatu iliyopita alifaa kuolewa na mchumbake wa miaka minane katika harusi iliyotarajiwa kufana sana.

Mume wake mtarajiwa ambaye alikuwa akifahamika kama Patty alikuwa ashamposa rasmi na hata kulipa mahari ya zaidi ya Sh1 milioni, na mipango ya harusi ilikuwa imekamilika.

Baada ya harusi, wawili hawa walitarajiwa kuhamia nchini Amerika ambapo kaka huyu alikuwa akifanya kazi ya udaktari.

Lakini ndoto hiyo ilikatizwa baada ya kaka kuugua ghafla na kuaga dunia, wiki mbili kabla ya harusi. Ni tukio lililowaacha jamaa na marafiki na simanzi tele huku wakishindwa kuelewa kwa nini mkasa huo umetokea.

Lakini hakuna aliyeathirika zaidi ya Betty ambaye tangu siku hiyo, mambo hayajawahi kuwa sawa.

Lakini ili kukabiliana na majonzi, amebuni mbinu ya kiajabu kumkumbuka Patty.

“Nimehifadhi picha za mchumbangu katika kila sehemu nyumbani kwangu. Kuanzia ukutani sebuleni, hadi kwenye zulia, picha ya Patty imechapishwa kwa kila kifaa. Hata pazia zangu zimeundwa kwa kitambaa rasmi kilichochapishwa picha zake.

Ukienda jikoni mambo ni yale yale. Sahani, vikombe, sinia na hata vitambaa vya kupangusa vyombo vimechapishwa picha yake Patty. Msalani pia kuna picha kubwa na kuta za bafu zina vigae maalum zilizojumuisha picha zke.

Katika chumba cha kulala mambo si tofauti. Shuka, blanketi, pazia, zulia, malapa na hata nguo zangu za kulala zimetawaliwa na picha ya Patty.

Video zetu nyakati tulipokuwa pamoja pia bado zipo ambapo kila jioni baada ya kazi, lazima nizitazame angalau nijikumbushe maisha tuliyokuwa nayo.

Isitoshe, picha zake ziko kwenye simu na mitandao ya kijamii. Kwenye Facebook bado namtambulisha kama mchumbangu katika ile sehemu ya uhusiano.

Kila Jumamosi mimi husafiri kwa muda wa saa nane kuelekea kwao alikozikwa nikiwa nimebeba maua ya kuweka kwenye kaburi lake.

Nikiwa hapo, hupewa kiti na kukesha pale na hakuna wikendi hata moja ambayo nimekosa ‘kumtembelea’.

Japo kuna wakati hutafakari kuendelea na maisha na hata kumruhusu mtu mwingine moyoni lakini pindi wanapokumbana na kumbukumbu zake kwangu, hunisepa.

Hii imewafanya wazazi na marafiki zangu kuingiwa na wasiwasi kwamba huenda nisiolewe.

Wanadhani kuwa nimepagawa lakini hawaelewi kuwa penzi letu lilikuwa la kipekee na kamwe hatuwezi kutenganishwa na kifo.

Naamini yu nami kila wakati na anatambua jitihada zangu za kudumisha kumbukumbu yake”.

You can share this post!

AKILIMALI: Kilimo cha ndizi ni chenye manufaa tele

CHOCHEO: Raha ya usingizi wa mahaba

adminleo