Makala

DAU LA MAISHA: Ugonjwa haujazima moyo wa ukarimu

October 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

LICHA ya kuwa anaugua kansa, amejitiwika jukumu la kusaidia wagonjwa na walioathirika kutokana na maradhi haya.

Ni shughuli ambayo Millicent Kagonga, 29, amekuwa akifanya kupitia Symbol of Hope Warriors, mradi alioanzisha Kariobangi North, jijini Nairobi.

Kupitia mradi huu alioanzisha miaka miwili iliyopita, ameweza kukusanya wanachama 40 waliosajiliwa kutoka mitaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kariobangi, Korogocho, na Dandora ambapo pamoja wamekuwa msaada kwa wagonjwa wengi wanaokumbwa na hali hii.

“Wanachama wa kikundi hiki wamepona kutokana na kansa au wangali wanakabiliana na maradhi haya,” aeleza Kagonga.

Shughuli zao zinahusisha kufanya kampeni za kukabiliana na unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa kansa.

“Tuligundua kwamba wagonjwa wengi huzidiwa na makali kwa sababu ya kutengwa ambapo kwa kuzungumzia suala hili katika jamii, vile vile kuwapa moyo kwa njia moja au nyingine tunawapa nguvu,” aeleza.

Sio hayo tu, kwani ili kukabiliana na unyanyapaa pia wamekuwa wakiwaandalia wagonjwa chakula na kujumuika nao. “Kutokana na vidonda vinavyohusishwa na maradhi haya, waathiriwa hutoa harufu mbaya na sio wengi ambao wangependa kula nao, na hivyo kwa kujumuika nao, tunawapa moyo,” asema.

Lakini pia shughuli zao zimekuwa zikihusisha kuwasaidia hospitalini.

“Tumeshuhudia visa vya jamaa za waathiriwa wakikataa kuchukua jukumu la kuwapeleka wenzao hospitalini, pengine kwa kuhofia gharama,” asema.

Pia wamekuwa wakiunganisha wagonjwa na mashirika ya kutoa usaidizi hasa wa kifedha ili kugharimia matibabu.

Hata hivyo, mchango mkuu umekuwa wa kuwasaidia kupata vifaa muhimu vya kimatibabu.

“Kwa mfano kuna wagonjwa wanaohitaji mifuko maalum ya kuhifadhi mkojo (colostomy bag) ambapo tumekuwa tukishirikiana na mashirika ya ufadhili kuhakikisha kwamba wanapata vifaa hivi. Kwa upande mwingine sisi kama wanachama, hushona matiti bandia, ambayo husambazwa miongoni mwa akina mama waliokatwa matiti kutokana na kansa ya matiti,” aeleza.

Katika kipindi cha miaka miwili ambayo wamekuwa wakishughulika, wamewafaa wagonjwa 35 kwa njia tofauti.

Haijakuwa rahisi kwa wanachama hawa.

“Katika harakati hizi tumepoteza kadha wa kadha, lakini tuliosalia, tunaendelea na safari,” aeleza.

Aidha, wamekuwa wakikumbana na changamoto ya ukosefu wa fedha hasa ikizingatiwa kwamba hawana ufadhili wowote.

“Kutokana na sababu kwamba wanachama wetu wanatoka katika mitaa ya vitongoji duni, hawana uwezo wa kifedha, ambapo wakati mwingine inatubidi kutegemea wahusika kutulipia nauli kuwapeleka hospitalini,” aeleza.

Lakini ili kuukabiliana na tatizo hili, wanajihusisha na miradi ya kujikimu kiuchumi kama vile kuunda mapambo ya vito, kuunda sabuni za maji, na kushona ponjo, bidhaa ambazo wao huuza na kupata pesa kidogo.

Bi Kagonga anasema kwamba azma yake ya kushughulikia wagonjwa wa kansa inatokana na sababu kwamba yeye pia ni mwathiriwa wa maradhi haya.

Akiwa na miaka miaka 20 pekee aligundua kwamba alikuwa na kansa ya mlango wa uzazi.

Hakuwa na pesa za kugharimia matibabu lakini alibahatika kupata mfadhili.

“Hii ilinifanya hata mimi nitake kusaidia wengine wanaokumbwa na maradhi haya,” aeleza.

Lakini jambo kuu lililomfanya kutaka kuanzisha mradi huu ni usaidizi aliopokea alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

“Mwanzoni nilipohitajika kuanza matibabu, sikuwa najua hata hospitali hii ilipo. Kwa hivyo, nilipata usaidizi mwingi kutoka kwa watu waliokuwa wakinielekeza, na hivyo pia mimi nataka kurudisha mkono kwa kuwafaa wengine. Aidha, hamu yangu ilitokana na upendo mwingi nilioonyeshwa na wagonjwa wengine hasa nikiwa hospitalini,” asema.

Kwa sasa anatumai watapata ufadhili utakaowasaidia kueneza shughuli hizi katika sehemu zingine nchini.