Habari Mseto

Mbuzi awazaa wanambuzi sita Mathira

October 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MKULIMA na mfugaji Mathira Mashariki, Kaunti ya Nyeri nusura aingie Kitabu cha Kumbukumbu cha Ulimwengu cha Guiness baada ya mbuzi wake kujifungua wanambuzi sita.

Huku wakiwa wameshangazwa na kisa hicho wakazi wa kijiji cha Miiri, kilichoko kilomita tano kutoka mjini Karatina wamekuwa wakifurika nyumbani kwa Bi Grace Muthoni, 51, kujionea “maajabu haya” kwa vile mbuzi huzaa wanambuzi pacha au watatu mara moja.

Wakati Taifa Leo ilifika kwa Bi Muthoni, alikuwa na kazi nyingi ya kuwapokea wageni na kuwahudumia wanambuzi hao.

Mfugaji huyo amesema alishangazwa na mbuzi wake kwa kuwazaa wanambuzi hao sita.

Alidokeza hapo awali alikuwa amezaa wanambuzi wane kisha wakafariki miaka sita iliyopita.

“Nilishtuka. Sikuamini wakati wanambuzi hawa walitoka mmoja baada ya mwingine hadi wakafika sita. Sijawahi shuhudia kisa kama hiki hapo mbeleni. Nimeuona muujiza na Baraka za Mungu kwa wakati mmoja,” alisema Bi Muthoni.

Hata hivyo Bi Muthoni anayefuga mbuzi wa kukamua maziwa amesema kizingiti kikubwa cha kumtunza mbuzi wake ni maradhi ya figo anayougua.

“Ninaugua maradhi ya figo na ninatoa wito kwa mtu anayeweza kunitolea figo moja kwa vile zangu zimeathiriwa na ugonjwa wa Kisukari ninaougua,” alirai Bi Muthoni.

Kulingana na nakala za Kitabu cha Guinness katika eneo la Arizona, Amerika ndiko mbuzi aliwazaa wanambuzi saba Februari 2019.

Kama sio mbuzi huyo, mbuzi wa Bi Muthoni angeliandikwa katika kitabu hiki lakini alishindwa na huyo aliyewazaaa wanambuzi saba kwa wakati mmoja.