• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Bobi Wine sasa akimbilia mataifa ya nje kumbandua Museveni

Bobi Wine sasa akimbilia mataifa ya nje kumbandua Museveni

Na DERICK WANDERA, DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

MWANASIASA msanii ambaye pia ni mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ameirai jamii ya kimataifa ifuatilie kwa makini uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Uganda mwaka 2021.

Uganda tayari inakabiliwa na masuala mazito ya ukiukaji wa haki za kibinadamu, serikali ya Rais Yoweri Museveni ikilaumiwa pakubwa kwa uongozi wa kiimla na ukandamizaji wa haki za wapinzani.

Kauli ya Bobi Wine inaajiri baada ya Rais Museveni kuwataja kama maajenti wa mataifa ya kigeni yenye nia ya kusambaratisha utawala wake.

Kupitia taarifa, Wine alimkashifu Rais Museveni kwa kudai kwamba wanatumiwa na maadui wa Uganda, akimkumbusha kwamba hata yeye alishirikiana na mataifa ya nje alipokuwa akishiriki vita vya kuingia afisini miaka ya 80.

“Kwa kweli nimetangamana na baadhi ya watu kutoka mataifa ya nje ambao walimsaidia Rais Museveni na kuingia mamlakani. Wengi wamenieleza kwamba wanajutia hatua yao baada ya Rais kukenguka na kuwa katili hasa kwa msingi wa kidemokrasia. Sasa wengi wao hawataki hata kushirikiana naye,” akasema Wine.

Aidha alimtaka Rais kumfichua jamaa ambaye alimpiga risasi dereva wake Yasin Kawuma wakati wa machafuko eneo la Arua huku pia akidai ni kiongozi huyo wa taifa ambaye anamiliki jumba ambalo wapinzani wa serikali wanaendelea kuteswa, baadhi wakiuawa.

Kumfungia nje

Bila kutoa maelezo mengi, mbunge huyo alidai kwamba serikali inapanga njama ya kutumia juhudi zote kumzuia kuwania kiti cha Urais kwenye uchaguzi huo wa 2021.

“Naendelea kuyaomba mataifa mengine ambayo ni marafiki wa Uganda kuwa makini na kufuatilia masuala yanayoibuka kabla ya uchaguzi mkuu. Sisi tupo tayari kushirikiana na wanaotakia taifa hili maendeleo na uongozi mzuri. Uchumi pekee haufai kutumiwa kama kigezo cha uhusiano kati ya Uganda na mataifa bali pia ushirikiano wa kisiasa na demokrasia kwa raia wake,” akaongeza.

Hata hivyo, mkurugenzi wa kituo kikuu cha uanahabari Uganda Kanali Shaban Bantariza alimtaka Wine ajihushishe na kijivumisha ili kupata mamlaka badala ya kuitisha msaada wa mataifa ya kigeni kuangazia matukio ya kisiasa katika nchi huru kama Uganda.

“Hii itamsaidia aje kutwaa mamlaka? Watu kutoka nje hawafai kuingilia masuala ya Uganda,” Kanali Shaban akasema kwenye mahojiano.

Waziri wa Habari na Mawasiliano Frank Tumwebaze naye alisema Wine anajisumbua bure kwa kuwa mataifa ya nje hayawezi kumsaidia kutimiza ndoto yake ya kuwa Rais wa Uganda.

  • Tags

You can share this post!

Mbuzi awazaa wanambuzi sita Mathira

Mvua iliyopitiliza kiwango yasababisha hasara tele

adminleo