• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Refarenda, usalama vyashamiri katika sherehe za Mashujaa Dei

Refarenda, usalama vyashamiri katika sherehe za Mashujaa Dei

Na WAANDISHI WETU

MAGAVANA Jumapili walitumia sherehe za Mashujaa Dei kupigia debe hitaji la marekebisho ya Katiba huku makamishna wa kaunti mbalimbali wakitumia nafasi hiyo kuhimiza umma kuhusu masuala ya usalama.

Ingawa Baraza la Magavana hivi majuzi lilizindua mchakato wa Ugatuzi Initiative kuhusu marekebisho ya Katiba wanayotaka, waliozungumza Jumapili walisema wataunga mkono ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) endapo itatoa mapendekezo ambayo yatasaidia kustawisha ugatuzi.

Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi alisema kufikia sasa amependezwa na lengo la BBI kuleta usawa na uwiano wa jamii na itakuwa vyema kama ripoti yao inayotarajiwa kutolewa wiki hii itapendekeza kwamba kila kaunti iwakilishwe katika serikali kuu mbali na kuongeza mgao wa fedha kwa kaunti.

“Tutaisoma kwa makini sana ili kubainisha kama italeta pesa mashinani la sivyo tuiangushe jinsi tulivyofanyia Punguza Mizigo,” akasema Murungi katika uwanja wa Kinoru.

Mwenzake wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana alisema ugatuzi umepiga hatua kubwa lakini marekebisho ya katiba yanahitajika kutatua vikwazo vilivyopo kaam vile ugavi wa rasilimali za kitaifa.

“Kwa hakika, ugatuzi unahusu wananchi,” akasema alipohutubu katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Muslim, katika Kaunti Ndogo ya Navakholo.

Katika Kaunti ya Vihiga, Gavana Wilber Ottichilo aliahidi kuhakikisha utawala wake umebuni sera itakayotambua na kutoa taadhima kwa mashujaa wanaotoka eneo hilo.

Hotuba ilisomwa kwa niaba yake na Naibu Gavana Patrick Saidi katika uwanja wa Municipal ulio Mbale.

Kwingineko Lamu, Kamishna wa Kaunti, Bw Irungu Macharia alitaka wananchi wawajibike zaidi kukabiliana na janga la mihadarati.

Alisema inasikitisha jinsi jamii imekuwa ikiwaruhusu walanguzi wa dawa za kulevya kuendeleza biashara yao bila kutatizwa.

Eneo la Nakuru, naibu kamishna wa Nakuru Mashariki Bw Johnstone Maina aliwaonya wamiliki wa majumba mjini Nakuru dhidi ya kukodi nyumba zao kwa wahalifu.

“Kuanzia leo hii, tukiwakamata wahalifu katika nyumba yako, ujue wewe pia kama mmliki tutakuweka katika kundi moja na wahalifu hao,” akasema akiongea katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru wakati wa hafla za Mashujaa alisema.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu, Kamishna wa Kaunti, Bw Abdirizack Jaldesa alionya kwamba mtu yeyote atakayepatikana akirandaranda karibu na maeneo ya kufanyia mitihani ya kitaifa atakamatwa.

Akihutubu katika uwanja wa 64 mjini Eldoret, Bw Jaldesa aliahidi pia kwamba kamati ya usalama itaimarisha usalama katika kaunti hiyo.

Visa vya uhalifu vimekuwa vikiongezeka mjini Eldoret ikiwemo wizi wa magari katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, kando na wizi wa mifugo ambao umekuwa ukitatiza wakazi kwa miaka mingi.

You can share this post!

Wazee mnaovuta bangi mnachangia vijana kupotoka –...

TAHARIRI: Sera kuhusu tuzo za taifa ziwe wazi

adminleo