Makala

DIMBA: Kipchoge, Kamworor na Brigid fahari halisi ya Kenya

October 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KENYA kwa sasa inajivunia wanariadha wanaoshikilia rekodi zote za dunia katika mbio za Nusu Marathon (kilomita 21) na Marathon (kilomita 42) kwa upande wa wanawake na wanaume.

Mnamo Oktoba 12, 2019, Eliud Kipchoge, 34, aliingia katika mabuku ya historia kwa kuwa binadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 kwa chini ya muda wa saa mbili aliposhiriki kivumbi cha INEOS 1:59 Challenge jijini Vienna, Austria.

Mbio hizi zilidhaminiwa na bilionea mzawa wa Uingereza, James ‘Jim’ Ratcliffe.

Bingwa huyu wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon alikamilisha kivumbi cha INEOS kwa muda wa saa 1:59:40.2, siku moja kabla ya Mkenya Brigid Kosgei kuvunja rekodi ya dunia kwa upande wa marathon ya wanawake.

Kosgei, 25, alikamilisha mbio za Chicago Marathon, Amerika kwa muda wa saa 2:14.04 na kuondoa dakika moja na sekunde 21 kutoka kwa rekodi ya miaka 16 iliyowekwa na Mwingereza Paula Radcliffe mnamo 2003.

Mafanikio ya Kipchoge na Kosgei yaliwafanya kuteuliwa kuwania mataji ya Wanariadha Bora wa Mwaka Duniani katika hafla itakayoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) mnamo Novemba 23, 2019 jijini Monaco, Ufaransa.

Kipchoge alivunja rekodi ya Dunia katika mbio za kilomita 42 mwaka jana kwa kukamilisha kivumbi cha Berlin Marathon kwa muda wa saa 2:01:39 nchini Ujerumani. Hata hivyo, nusura rekodi yake hiyo ifutiliwe mbali na Mwethiopia Kenenisa Bekele, 37, aliyekamilisha mbio za Berlin Marathon kwa muda wa saa 2:01:41 nchini Ujerumani mnamo Oktoba 5, 2019.

Akichukuliwa kuwa mkimbiaji bora zaidi katika historia ya marathon, Kipchoge anajivunia ushindi katika makala 12 ya marathon kati ya 13 ambayo ameshiriki kufikia sasa.

Hambourg Marathon ilikuwa ya kwanza kabisa kwa Kipchoge kushiriki mnamo 2013.

Ushindi wa kwanza katika mbio hizo ulimjia mnamo 2014 katika Chicago Marathon. Hadi alipoweka rekodi mpya katika mbio za marathon, ndiye aliyekuwa mfalme mara tatu wa London Marathon na Berlin Marathon.

Mnamo Septemba 15, 2019, bingwa mara tatu wa riadha za Nusu Marathon Duniani, Geoffrey Kamworor, 26, aliweka rekodi mpya ya dunia katika mbio za kilomita 21 baada ya kutwaa taji la Copenhagen Half Marathon kwa muda wa dakika 58:01 nchini Denmark.

Alitia mfukoni kima cha Sh1 milioni kwa ushindi huo, Sh1 milioni nyinginezo kwa kuvunja rekodi ya dunia, Sh520,000 kwa kusajili rekodi mpya ya Copenhagen Half Marathon na kujizolea Sh207,000 za ziada kwa kukamilisha umbali huo chini ya muda wa dakika 60.

Hadi Kamworor alipotawala mbio za Copenhagen, Mkenya Abraham Kiptum ndiye aliyekuwa mshikilizi wa rekodi ya Dunia ya Half Marathon baada ya kukamilisha mbio hizo za kilimota 21 kwa muda wa dakika 58:18 jijii Valencia, Uhispania mnamo Oktoba 28, 2018.

Kamworor aliyebeba mataji ya dunia ya Half Marathon mnamo 2014, 2016 na 2018, alijibwaga uwanjani kwa minajili ya mbio za Copenhagen akijivunia muda bora zaidi katika nusu marathon wa dakika 58:54 alioutumia kujitwalia taji la Ras Al Khaimah mnamo 2013. Mbali na kuvunja rekodi ya dunia, Kamworor pia alifuta rekodi ya Copenhagen Half Marathon ya dakika 58:40 iliyowekwa na mwanariadha mzawa wa Kenya na raia wa Bahrain, Abraham Cheroben mnamo 2017.

Kabla ya Kamworor, Bedan Karoki, James Wangari na Daniel Kipchumba ndio Wakenya wengine waliowahi kutwaa mataji ya Copenhagen Half Marathon mnamo 2015, 2016 na 2018 mtawalia.

Joyciline Jepkosgei ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 10, aliweka rekodi mpya ya Nusu Marathon kwa kukamilisha mbio hizo za kilomita 21 jijini Valencia, Uhispania kwa muda wa saa 1:04:51 mnamo Oktoba 22, 2017.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 26, aliweka rekodi ya Dunia ya mbio za kilomita 10 (dakika 29:43) katika Jamhuri ya Czech mwaka 2018.

Alirejesha taji la New York City Half Marathon nchini Kenya baada ya kushinda mbio hizo za kilomita 21 nchini Amerika mapema mwaka 2019.

Wanawake wengine kutoka Kenya waliowahi kung’aa katika mbio za New York Half Marathon ni Catherine Ndereba (2006, 2008), Hilda Kibet (2007) na Caroline Rotich (2011, 2013).

Mwanariadha bora

Mbali na Kipchoge na Kosgei, Wakenya Beatrice Chepkoech, Hellen Obiri na Timothy Cheruiyot ndio wanariadha wengine ambao wameorodheshwa kuwania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka 2019.

Chepkoech, 28, ndiye bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji.

Zaidi ya kutia kapuni ubingwa wa mbio za Diamond League msimu huu, alitawala mashindano saba kati ya manane aliyoyashiriki mwaka 2019.

Muda wa dakika 8:57.84 aliouandikisha katika Riadha za Dunia zilizokamilika majuzi jijini Doha, Qatar ulimvunia nishani ya dhahabu.

Aliboresha rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi kwa sekunde nane mnamo 2018 kwa kukamilisha Herculis Diamond League kwa muda wa dakika 8:44.32. Kwa sasa, anashikilia rekodi ya mbio hizo aliyoiweka jijini Monaco, Ufaransa mnamo Julai 2018.

Kiini cha kuteuliwa kwa Obiri, 29, ni ufanisi aliojivunia katika Mbio za Nyika za Dunia jijini Aarhus, Denmark mwanzoni mwa mwaka huu kabla ya kunyanyua medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 katika Riadha za Dunia za Qatar kwa muda wa dakika 14:26.72. Awali, alikuwa amesajili muda bora wa dakika 14:20.36 aliposhiriki mbio hizo jijini London, Uingereza mnamo 2017.

Cheruiyot, 23, alitwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar. Cheruiyot aliyetawazwa bingwa wa Diamond League mnamo 2017, 2018 na 2019, amewahi pia kunyakua nishani ya fedha katika mbio za mita 1,500 wakati Riadha za Dunia zilipoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.

Hadi kutuzwa kwa Kipchoge mnamo 2018, mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 800 David Rudisha, 30, ndiye aliyekuwa Mkenya wa pekee kuwahi kuibuka Mwanariadha Bora duniani aliponyakua taji la mwaka 2010 tangu hafla ya kutuzwa kwa wanariadha bora ianzishwe mnamo 1988.