Vijana mahiri katika uopoaji miili majini
Na MERCY MWENDE
NI nadra kumpata binadamu ambaye anaweza kuhatarisha maisha yake ili kumwokoa mja mgeni kwake.
Hata hivyo, mjini Nyeri kipo kikundi kinachojulikana kama Nyeri Chania Divers ambacho kimejitolea kuopoa miili ya waliozama kwenye mabwawa na mito.
Nyeri Chania Divers ni kikundi cha wapiga mbizi 16 ambao walijumuika mnamo Julai 2015 baada ya kusaidiana kutafuta mwili wa mmoja wa wanakijiji wao ambao ulidaiwa kuwa ulikuwa umetupwa katika mto wa Chania.
Bw Patrick Gikaria, ambaye ni mwenyekiti wa kikundi hicho alieleza kuwa walisaidiana kama marafiki kutafuta mwili huo ambao walipata kuwa ulikuwa umefungiwa kwenye jiwe ili kuongezea uzito.
“IIikuwa ni vigumu kutambua mahali halisi ambapo mwili huo ulizama kwa sababu ya mikondo mingi iliyokuwepo ya maji,” alieleza.
Baada ya kuupata waliamua kuungana na kusajili kikundi hicho ambacho kilikuwa na wanachama 70 lakini wengi waliondoka baada ya kugundua kuwa hawakuwa magwiji wa kuogelea kama walivyodhania. Kikundi chenyewe kilianzishwa na lengo la kusaidia jamii, hivyo basi huwa hakilipishi huduma hiyo jamii.
“Mara nyingi jamaa ya wanaokumbwa na janga hili hawawezi kumudu kulipia huduma za wapiga mbizi wataalamu,” mwenyekiti alieleza.
Wengi wa wanachama wa kikundi hicho wako kati ya umri wa miaka 25 na 35 isipokuwa mwenyekiti wao Bw Gikaria. Bw Gikaria, 56, alitueleza kuwa hakuna mmoja kati yao ambaye amesomea ustadi huo.
“Wengi wetu tumelelewa vijijini hivyo basi tulipata fursa ya kuogelea kwenye mito na kujifunza ustadi huu,” Bw Gikaria alieleza.
Hata hivyo, aliwaonya vijana wanaokwenda kuogelea kwenye mito bila ujuzi kwani jambo hilo ndio sababu kuu inayochangia vifo kwenye mito katika eneo la Nyeri.
Mwenyekiti huyo alisema tangu mwaka wa 2015 wametoa zaidi ya miili 20, na mwaka 2019 wametoa miili 10.
“Wakati mwingine huwa tunaitwa kutoa miili ya watu inayoonekana ikielea juu ya maji, ingawa visa kama hivyo inabidi tuwajulishe polisi,” Bw Gikaria alieleza. Kikundi hicho kimeokoa miili katika mabwawa ya Hohwe na Kionywe na katika mito ya Sagana na Chania.
Wapiga mbizi hao walieleza kuwa wakiwa kwenye operesheni hiyo huwa wanapitia changamoto mbalimbali ikiwemo kujihatarisha na magonjwa kama Nimonia na Pumu kwa sababu hawana uwezo wa kununua mavazi ya kujikinga.
Wakati mmoja kikundi hicho kililazimika kuogelea katika Mto Sagana ulio katika kaunti ya Murang’a ambao una wanyama hatari wakitafuta mwili wa kijana aliyedaiwa kuanguka na pikipiki yake kwenye mto.
Wakati wa mvua, mto hufurika na maji kuchafuka hivyo basi inakuwa vigumu kwao kufanya mazoezi.
Uhaba wa pesa ili kuendeleza kikundi hicho ni jambo lingine ambalo limewakumba wapiga mbizi hao.
“Wengi wetu tunajimudu maishani na kazi ya ukulima, uwashi, ukondakta na uendeshaji wa bodaboda, hivyo hatuna uwezo wa kununua mavazi ya wapiga mbizi,” Mwenyekiti alieleza.
Ingawa kazi hii wanaifanya kwa muda maalum, nyakati zingine wanachama hao hulazimika kutafuta mwili kwenye mito kwa muda wa wiki mbili, hivyo wanalazimika kuwacha kazi zao za kudumu maishani.
Hawajaweza kujenga ofisi ambayo wanaweza kupeana huduma zao kwa urahisi, hivyo basi wao huwasiliana na jamii kupitia kwa mwenyekiti wao.
“Kunapotokea jambo, mimi huwasiliana na wanachama wenzangu kupitia kwa simu na kuwakusanya ili kuwatayarisha kwa operesheni,” Bw Gikaria alieleza.
Bw Samuel Kaiti, ambaye ni mmoja wa wanachama alieleza kuwa jambo lingine ambalo limewakuza kama kikundi kando na talanta walio nayo, ni shauku la kujitolea kusaidia jamii.
Alisema pia sera ingine ambayo imewakuza ni urafiki mkubwa baina yao hivyo basi kila mmoja ana wajibu wa kumtunza mwenzake wanapokuwa wakiogelea.
Bw Gikaria alieleza kuwa kazi yake katika operesheni hizo ni kuratibu na kuhakikisha kuwa kila mwogeleaji ako salama.
Mmoja wa waogoleaji hao Bw Dennis Maina, aliwashauri vijana wenzake kuwa wasichague kazi ila watumie talanta zao kujikuza kibinafsi na kusaidia wengine kwani waweza pata bahati siku moja.