NGILA: Vizingiti vya ustawi wa teknolojia ya dijitali viondolewe
Na FAUSTINE NGILA
KULINGANA na ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2019 kuhusu hali halisi ya uchumi wa kidijitali, Kenya ina mengi ya kujivunia ikilinganishwa na mataifa mengine barani Afrika.
Takwimu katika ripoti hiyo zinaonyesha kuwa taifa hili linaongoza duniani kwa idadi ya watu wanaotumia programu za simu kutuma, kupokea na kukopa pesa.
Kuna watumizi milioni 47 wa simu nchini, ambao ni asilimia 90 ya Wakenya ambao hutumia simu zao kuwasiliana kupitia sauti, arafa na Intaneti.
Sekta ndogo ya dijitali imekua kwa kasi zaidi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuvutia wawekezaji wa humu nchini na wa kigeni, ambao wamewekeza Sh34 bilioni.
Licha ya mfumo wa M-Pesa kushirikisha Wakenya wengi katika umiliki wa akaunti za benki kidijitali, bado kuna wananchi 12.7 milioni ambao hawajui maana ya kuwa na akaunti ya kuhifadhi hela.
Bado Kenya haijafikia kiwango kilichowekwa kimataifa cha gharama ya chini ya Intaneti ya asilimia mbili ya mshahara wa kila mwezi.
Gharama hii ni asilimia nne ya ujira hapa nchini.
Juhudi za serikali kusajili wananchi kwenye mfumo wa utambulisho wa kidijitali wa Huduma Namba ulikumbwa na visiki vingi, na ndio maana asilimia 38 ya Wakenya bado hawana vitambulisho.
Baada ya kuzindua mtaala mpya wa elimu, serikali imesifiwa na kukejeliwa kwa viwango sawa.
Wengi wa wakosoaji wameishangaa serikali kukosa kuweka somo la kidijitali kwenye mtaala, kama mataifa ya China, Amerika na Uingereza.
Dunia inapojiandaa kwa Mageuzi ya Nne ya Kiuchumi, Kenya imeshuhudia pengo kubwa katika taaluma za sayansi ya data, teknolojia ya kiotomatiki na Blockchain, ambalo serikali inajikokota kuziba.
Ripoti ya GSMA ya Septemba ilionyesha kuwa Kenya ina mazingira bora ya kukuza teknolojia Afrika inafaa kututia moyo, lakini ripoti hii ya Benki ya Dunia inafaa kutufungua macho ili kuboresha sehemu ambazo zinaonekana kutulemea.
Kwa mfano, kasi ya Intaneti mashambani inafaa kuongezwa kwa ushirikiano wa serikali na kampuni za simu, ili kuvutia uwekezaji kwenye kaunti.
Vituo vya ubunifu vinafaa kutengewa fedha na Wizara ya Teknohama, ili kupiga jeki juhudi na talanta za vijana wanaolenga kutumia teknolojia kuchangia katika kukuza uchumi.
Na mbona basi somo la teknolojia lisiwe la lazima kuanzia chekechea hadi chuo kikuu?