• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Mfalme amtema mpenziwe kwa kumdunisha mkewe

Mfalme amtema mpenziwe kwa kumdunisha mkewe

Na MASHIRIKA na MARY WANGARI

BANGKOK, THAILAND

MFALME wa Thailand Maha Vajiralongkorn amempokonya mpenzi wake vyeo na hadhi za kijeshi kwa kukosa uaminifu akimshutumu kwa kujaribu kudunisha nafasi ya mke wake rasmi, malkia wa nchi hiyo, kwa manufaa yake binafsi.

Amri ya kifalme kutoka kwa mfalme huyo mwenye umri wa miaka 67 iliyotangazwa Jumatatu ilijiri miezi mitatu tu baada ya kumpa Sineenatra Wongvajirabhakdi mwenye umri wa miaka 34 cheo cha mke na kufufua utamaduni wa jadi kwenye kasri wa kuoa mke mdogo.

Sineenatra alipokonywa cheo chake cha Chao Khun Phra Sineenatra Bilasakalayani pamoja na vyeo vyake na hadhi ya kifalme na kijeshi.

Mnamo Mei, mfalme alimtaja mpenzi wake wa muda mrefu Suthida Vajiralongkorn Na Ayudhya kama malkia wake walipoana siku chache kabla ya kutawazwa kama mfalme.

Vajiralongkorn alichukua kiti cha ufalme 2016 kufuatia kifo cha babake Mfalme Bhumibol Adulyadej, aliyetamalaki kwa miaka 70.

Amri ya Jumatatu ilimkashif vikali Sineenatra ikitaja vitendo vyake kama “vinavyochukuliwa kama utovu wa heshima, kukosa shukurani, kupuuza ukarimu wa kifalme, kusababisha migawanyiko baina ya wahudumu wa ufalme, kusababisha hali ya kukosa kuelewana miongoni mwa watu na kudunisha taifa na ufalme”.

Wawili hao, Suthida mwenye umri wa miaka 41 na Sineenatra wamehudumu kama maafisa wakuu katika vitengo vya usalama vya kasri.

Awali Suthida alikuwa mhudumu wa ndege katika Shirika la Ndege la Thai Airways, huku Sineenatra akiwa muuguzi wa jeshi.

Vajiralongkorn ana watoto saba kutoka ndoa za awali ambazo zote zimeishia kwa talaka.

Amri ya kifalme ilichukua hatua zisizo za kawaida kufafanua sababu za kuchukua hatua hiyo dhidi ya Sineenatra.

Ilimshutumu dhidi ya kukosa nidhamu kwa kujitahidi kuzuia uteuzi wa Suthida kama malkia ili yeye atwae nafasi hiyo ambapo baada ya kushindwa kumzuia hasimu wake, “tamaa yake na malengo” yakamsababisha kuendelea kutafuta mbinu za kujipandisha cheo.

Kulingana na taarifa, mfalme alijaribu kutuliza mambo na kuondoa shinikizo kwenye ufalme kwa kumteua Sineenatra kama mpenzi wake rasmi kifalme.

Hata hivyo, taarifa ilisema “Hakutosheka na hadhi ya ufalme aliyotwikwa na bado akatia kila juhudi kuwa sawa na malkia.”

You can share this post!

Ahamia kwa demu kuhepa mke kelele

KAWIRA: Anawanasua vijana kutoka kwa ulevi

adminleo