Habari Mseto

Kenya kuwa mwenyeji wa hafla ya WPF

October 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

KENYA itakuwa mwenyeji wa hafla ya kwanza ya World Poverty Forum (WPF) itakayofanyika mnamo Januari mwakani.

Hafla hiyo itaandaliwa katika mtaa wa Kibera ambao unajulikana kama mmojawapo wa makazi makubwa ya madongoporomoka barani Afrika.

Mmoja wa waandalizi wa shirika la Shining Hope for Communities (Shofco) ambaye anahusika na maandalizi ya hafla hiyo Bw Kennedy Odede alisema kuwa hafla hiyo ya siku mbili inuia kutafuta njia mwafaka za kukabiliana na umaskini.

“Tutawaleta viongozi kutoka sehemu mbalimbali ili waweze kujionea wenyewe hali ya umaskini na jinsi ambavyo hali hii inaweza kubadilika kupitia ujima wa mashirika mbalimbali,” akasema Bw Odede.

Kulingana na Bw Odede, hafla hiyo pia itawapa sauti wakazi wa mitaa duni kutoa dukuduku bila uoga.

“Sehemu ambapo hafla hiyo itaandaliwa ina umuhimu zaidi kwani ni tofauti na dhana ya kuwa mikutano aina hiyo inapaswa kufanyika katika hoteli kubwa za kifahari ambapo idadi kubwa ya wasiojiweza hushindwa kuhudhuria,” aliongeza Bw Odede.

Katika hafla hiyo, pia kutakuwa na uzinduzi wa mradi wa Global Alliance for the Poor.