Safari ya Raila, Uhuru kwenda nchini Urusi kuchelewesha ripoti ya BBI
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM, Raila Odinga, wamealikwa kuhudhuria kongamano la kibiashara kati ya Urusi na Afrika litakalofanyika leo na kesho, siku ambayo walitarajiwa kukabidhiwa ripoti ya Jopo la Uwiano (BBI).
Kuungana kwao katika kongamano hilo kunamaanisha kuwa Wakenya watasubiri kabla ya kujua rasmi mapendekezo ya BBI ambayo viongozi hao wamekuwa wakipigia debe hata kabla haijatolewa.
BBI ilitarajiwa kuwakabidhi viongozi hao ripoti hiyo Alhamisi, Oktoba 24, 2019, tarehe ya mwisho iliyopaswa kukamilisha majukumu yake.
Rais Kenyatta aliondoka nchini baada ya kuongoza taifa kuadhimisha sikukuu ya Mashujaa mnamo Jumapili iliyopita jijini Mombasa na kwenda Japan kwa sherehe ya kutawazwa kwa Mfalme Naruhito.
Baada ya sherehe hiyo, Rais Kenyatta alitarajiwa kuelekea jiji la Sochi nchini Urusi kuungana na marais wengine zaidi ya 50 wa bara Afrika kwa kongamano la kwanza la kibiashara kati ya Urusi na Afrika.
Bw Odinga naye alitarajiwa kuhudhuria kongamano hilo katika wadhifa wake wa mjumbe maalumu wa Muungano wa Afrika kuhusu miundomisingi.
“Anatarajiwa kusafiri kwenda Urusi lakini hajaondoka bado. Anapaswa kuungana na viongozi wengine katika kongamano la kibiashara la Afrika na Urusi,” alisema afisa mmoja katika ofisi ya Bw Odinga.
Raila kuhutubu
Kulingana na waandalizi, Bw Odinga atakuwa mmoja wa watakaohutubu katika kikao kimoja cha kongamano hilo la siku mbili, ambalo wageni zaidi ya 3,000 wanatarajiwa kuhudhuria wakiwemo wafanyabiashara watajika barani Afrika.
Kutoka Kenya, mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara Richard Ngatia na mfanyabiashara maarufu Vimal Shah ni miongoni mwa walioalikwa.
Kongamano hilo limeandaliwa na wakfu wa Roscongress Foundation na litaongozwa kwa pamoja na Rais wa Urusi, Vladimir Putin na mwenzake wa Misri, Abdel Fattah El Sisi, ambaye ni mwenyekiti wa Muungano wa Afrika (AU).
Kama kawaida yake anapohudhuria mikutano kama hiyo, ujumbe wa Rais Kenyatta utakutana na kushauriana na maafisa wa Urusi katika juhudi za kukuza uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara kati ya nchi hizi mbili.