• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
TAHARIRI: Hatua ya Trump ni muhimu kwa Kenya

TAHARIRI: Hatua ya Trump ni muhimu kwa Kenya

Na MHARIRI

HATUA ya utawala wa Rais Donald Trump wa Amerika kutangaza msururu wa vikwazo kwa Wakenya wanaoshukiwa kushiriki katika maovu mbalimbali ya kijamii, yakiwemo ufisadi na uuzaji wa mihadarati, ni nzuri na bila shaka itasaidia kukabili uhalifu nchini.

Kwa miaka mingi, viongozi wa tabaka mbalimbali, wakiwemo wanasiasa wa ngazi za juu, wamekuwa wakipora mali ya umma na kusafirisha baadhi ya mapato hayo hadi mataifa ya magharibi ambapo wanawekeza.

Sasa, huenda hilo lisiwezekane endapo serikali ya Amerika itatekeleza kipengele kwenye sheria zake ambazo zinawapa mamlaka wakuu nchini humo kupiga marufuku washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati kuingia nchini humo.

La muhimu zaidi ni kwamba, wale wanaotumia mamlaka yao vibaya na kupora fedha za umma kisha wanasafiri Amerika na kwingineko Ulaya kufurahia matunda ya wizi sasa hawatafanikiwa kufanya hivyo.

Kama alivyosema balozi wa Amerika nchini Kyle McCarter, viongozi hao laghai wanaofyonza Wakenya kisha wanapeleka watoto wao katika vyuo vikuu nchini humo sasa hawatapata nafasi ya kufanya hivyo.

Tunapongeza balozi huyo kwa hatua yake ya kukosoa na kuchukua hatua. Kwa mfano, baada ya kutambua udhaifu katika mfumo mzima wa kuwashtaki wahalifu wanaopora mali ya umma, serikali ya Amerika iliamua kuwapa mafunzo waendesha mashtaka kadha.

Miezi minne iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kupeleleza Uhalifu (DCI) George Kinoti na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji walifanya mashauriano ya kina na kuanzisha ushirikiano mpya na Shirikisho Kuu la Upelelezi wa Jinai Amerika (FBI).

Ni kupitia kuimarisha asasi zilizotwikwa jukumu la kukabiliana na wizi wa fedha za umma ambapo uhalifu kama huo utakomeshwa.

Kila taifa rafiki kwa Kenya lina jukumu la kuisaidia kwa hali na mali kuangamiza ufujaji wa fedha za umma unaotekelezwa na wachache ambao hatimaye huficha mabilioni hayo ng’ambo ama kuwekeza katika elimu ya watoto wao.

You can share this post!

Safari ya Raila, Uhuru kwenda nchini Urusi kuchelewesha...

MATHEKA: BBI si ya kusaidia raia, ni ya kufaa wanasiasa

adminleo