Naibu Mwalimu Mkuu na mwenzake wakamatwa kwa kumnajisi mwanafunzi Murang'a
Na NDUNGU GACHANE na CHARLES WASONGA
NAIBU mwalimu mkuu na mwalimu mmoja wa Shule ya Upili ya Ndutumi, Kaunti ya Murang’a wamekamatwa kwa tuhuma za kumnajisi mwanafunzi wa kidato cha kwanza.
Kulingana na Afisa wa Upelelezi wa Jinai kaunti ya Murang’a Julius Rutere, Naibu huyo wa Mwalimu Mkuu alimdhulumu kimapenzi mwanafunzi huyo wa kike.
Lakini mwanafunzi huyo aliporipoti kwa mwalimu msimamizi wa darasa, mwalimu huyo pia alimgeuka na kumnajisi mara kadhaa.
Afisa huyo wa upelelezi alisema walimu hao wawili watashtakiwa katika mahakama ya Murang’a leo Jumatano kwa kosa la kumnajisi mtoto huyo wa umri mdogo.
“Watashtakiwa mahakama wa unyama huo. Ukaguzi umefanywa na kubaini kwua msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 alinajisiwa vibaya zaidi,” Bw Rutere akaambia Taifa Leo.
Alilaani kitendo hicho akisema inasikitisha kuwa walimu ambao wametwikwa wajibu wa kuwalinda wanafunzi lakini wanawageukia na kuwadhulumu kingono.
“Wazazi wamewapa walimu watoto wao ili wawafunze na kuwa vielelezo vyao. Lakini inasikitika kuwa baadhi ya wanawadhulumu kinyama,” akasema Bw Rutere.
Kisa hicho kilitokea Jumapili saa kumi za jioni wakati wanafunzi wanaosoma na kuenda nyumba walikuwa wameondoka na wale wa mabweni walikuwa wakishiriki michezo.
Naibu huyo wa Mwalimu Mkuu alikuwa amemshauri mwanafunzi huyo kusalia darasani wakati alipodaiwa kutenda kitendo hicho.