• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Raia wasubiri matokeo baada ya uchaguzi wa urais

Raia wasubiri matokeo baada ya uchaguzi wa urais

Na AFP

RAIA wa Botswana wanaendelea kusubiri matokeo ya Urais baada ya kuingia debeni Jumatano kushiriki uchaguzi mkuu ulioshirikisha wawaniaji wa Urais na viti vya ubunge.

Ushindani mkali unatarajiwa kati ya Rais wa sasa Mokgweetsi Masisi na kiongozi wa upinzani Duma Boko.

Raia jana walifika katika vituo mbalimbali vya upigaji kura kushiriki uchaguzi huo ambao wadadisi wanasema huenda ukashuhudia chama tawala cha taifa hilo BDP kikishindwa na kile cha upinzani cha UDC.

Maelfu ya raia jana walifika kwenye vituo vya upigaji kura kuanzia saa 12 asubuhi kushiriki kwenye zoezi hilo muhimu la kidemokrasia baadhi wakieleza waziwazi kiongozi ambaye wanampigia upato. Katika mji mkuu wa Gaborone, wapigakura walifika katika shule ya upili ya Tlogatioga mkesha wa siku ya uchaguzi wakisubiri kutekeleza wajibu huo muhimu.

“Mimi nimeshaamua kiongozi nitakayempigia kura na nimekesha hapa ili kuhakikisha nimetimiza hilo. Hata hivyo, hawanii kupitia chama ambacho nimekipigia kura kwenye chaguzi zilizopita,” akasema Chops Maswikiti, 37 ambaye ni mfanyakazi wa benki.

Rais Masisi ambaye aliingia mamlakani mwaka jana baada ya aliyekuwa Rais Ian Khama kustaafu atakuwa na kibarua kigumu cha kuchaguliwa ikizingatiwa mtangulizi wake ameshakigura chama tawala na sasa anamuunga mkono Boko.

Rais mstaafu Khama aliondoka BDP mnamo Mei mwaka huu akimshtumu Rais Masisi kwa kiburi na majitapo huku akirejelea chama tawala kama kilichokufa chini ya utawala wa muda mfupi wa kiongozi huyo.

Kitovu cha demokrasia

Ingawa Botswana imetajwa kama kitovu cha demokrasia barani Afrika, kura hiyo huenda ikashuhudiwa BDP ambayo imeongoza tangu nchi hiyo ijinyakulie uhuru miaka 53 iliyopita, ikiingia upinzani.

“Uongozi wa Rais Masisi ni tisho kwa demokrasia ya taifa hili. Litakuwa jambo jema kwa demokrasia yetu iwapo taifa hili litaongozwa na chama kingine,” akasema Khama wakati wa mkutano wa mwisho mjini Mahalapye ambao ni kilomita 200 kutoka mji wa Gaborone.

Wakati huo huo, Rais Masisi akihutubia mkutano wake wa mwisho wa hadhara katika kijiji chake cha Moshupa alikanusha kwamba tayari amefunganya virago ofisini mwake baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa ushindi.

“Sijafunganya virago ofisini mwangu na bado sijaondoka katika Ikulu. Hata hivyo, iwapo nitashindwa nitafunganya virago taratibu na kuelekea nyumbani kwangu. Sheria ndiyo hutoa mwongozo wa kila suala hapa Botswana,” akasema Rais Masisi.

You can share this post!

Bima ya Afya: Jubilee iliwahadaa wakongwe mwaka 2017?

AKILIMALI: Vijana wabuni ajira kwa kusaga unga wa ndizi

adminleo