Ziwa Victoria hatarini
Na MAGDALENE WANJA
ZIWA Victoria limetambulika kama ‘moyo’ wa bara la Afrika na ni chanzo cha mto mrefu zaidi wa Nile.
Ingawa ziwa hilo lina samaki wengi wa aina mbalimbali, linaendelea kukabiliwa na hatari kubwa ya kukauka (silting).
Kulingana na mwanasayansi Dkt David Langat kutoka shirika la Kenya Forestry Research Institute (KEFRI), zaidi ya tani 3 milioni za mchanga huingia kwenye ziwa hilo.
“Ziwa hilo linakabiliwa na changamoto tele zikiwemo uchafuzi wa mazingira, uvamizi kutoka kwa mimea hatari na uchafu wa udongo ambao unachangia pakubwa katika uharibifu,” alisema Dkt Langat.
Habari hii inasisitiza ripoti ya hivi punde ya muungano wa International Union for Conservation of Nature (IUCN) ambayo inasema kuwa asilimia 76 ya wanyama katika maeneo ya maziwa yako katika hatari ya kuisha duniani.
Ripoti hiyo ya 2018 kwa jina ‘Freshwater Biodiversity in the Lake Victoria Basin Faces Extinction’ ilihusisha hatari hiyo na uchafuzi wa mazingira, njia haribifu za ukulima na kuwepo kwa mimea hatari katika ziwa hilo.
Aliongeza kuwa mmonyoko unaoelekeza ziwani udongo ulianzia miaka ya 1970 na unaendelea kuwa mbaya zaidi kutokana na ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Ziwa Victoria ni la pili kwa ukubwa duniani kuzingatia kigezo cha upana wake mraba (surface area).