Yatani aomba seneti kuidhinisha mkopo wa hadi Sh9 trilioni
Na CHARLES WASONGA
KAIMU Waziri wa Fedha Ukur Yatani ameitaka seneti kuunga mkono pendekezo la serikali la kutaka iruhusiwe kuchukua mikopo ya hadi Sh9 trilioni kutoka kiwango cha sasa cha Sh6 trilioni.
Alisema ikiwa ombi la Wizara ya Fedha kutaka sheria ibadilishwe ili iweze kukopa kiwango hicho cha fedha halitapitishwa, huenda shughuli za serikali zikakwama kwani chini ya sheria za sasa haiwezi kukopa zaidi ya Sh6 trilioni.
Akiongea Jumatano alipofika mbele ya kamati ya pamoja ya seneti kuhusu sheria mbadala na Fedha na Bajeti Bw Yatani alisema wakati huu serikali haiwezi kutenga fedha za kufadhili miradi ya maendeleo kwa sababu haiwezi kukopa zaidi.
Bw Yatani alitoa mfano wa Mpango wa Serikali wa Utoaji Huduma za Matibabu kwa Wote (UHC), usambazaji wa stima mashinani na ile ya miundombinu kama baadhi ya miradi ambayo itaathirika kutokana na uhaba wa pesa ikiwa serikali haitaruhusiwa kukopa zaidi.
“Nawaomba enyi maseneta muidhinishe mabadiliko kwa sheria ya usimamizi wa fedha ili tuweze kukopa hadi Sh9 trilioni, walivyofanya wenzenu wa Bunge la Kitaifa wiki jana. Ikiwa mtakataa ombi hili, basi tutatumbukia kwenye shida kubwa kama taifa kwani hatuna njia nyingine ya kupata hela,” akasema alipokuwa akimjibu Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot aliyetaka kujua kile kitafanyika ikiwa seneti itakataa ombi hilo.
Bw Cheruiyot alionya serikali dhidi ya kuendeleza mtindo wa kuweka mipango ya matumizi ya fedha ilhali haina fedha hizo wala haijui itakakozipata.
“Bw Waziri, huenda tunataka kuwaunga mkono katika utekelezaji wa miradi inayoendelea, lakini mtindo wa kuanza kukopa ili kuanzisha miradi mipya hairuhusiwi,” akaonya.
Katika barua iliyotuma kwa seneti mnamo Oktoba 15, 2019, Wizara ya Fedha iliiomba seneti kukubali kuidhinisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Serikali Kuu, kanuni ya 2015, sehemu ya 26 (1) (c).
Waziri anataka kanuni ya 26 (1) ilifanyiwe mabadiliko kwa kufuta maneno “asilimia 50 ya Jumla ya Utajiri wa Nchini (GDP) katika thamani halisi ya sasa.”
Kiwango cha madeni ya Kenya kilifikia Sh6 trilioni mnamo Agosti 2019 baada ya taifa hili kukopa Sh200 bilioni zaidi ndani ya kipindi cha miezi miwili. Lakini sasa Wizara ya Fedha inataka iruhusiwe kukopa Sh3 trilioni zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa chini ya sheria ya sasa.
Chini ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Serikali ya 2015, inayotumika sasa, serikali inaruhusiwa kukopa hadi asilimia 50 ya GDP pekee. Lakini wiki mbili zilizopita, wabunge wa bunge la kitaifa waliifanyia mageuzi sheria hiyo na kuweka kiwango hicho kuwa Sh9 trilioni kama ilivyopendekezwa na Wizara ya Fedha.
Kutekeleza ajenda za serikali
Jumatano Yatani alisema kiwango hicho cha mkopo kitaweza kuisaidia serikali kutekeleza ajenda zake za maendeleo na katika kiwango ambacho itaweza kumudu kulingana na matakwa ya Katiba.
Vilevile, alisema mageuzi ya sheria hiyo yataiwezesha serikali kukopa pesa za kuiwezesha kulipa mikopo ya riba ya juu huku ikichukua mikopo ya inayotozwa riba ya chini na ambayo inaweza kulipiwa kwa kipindi kirefu.
“Tunafanya hivi kwa nia njema kwa sababu tutaelekea pabaya, ikiwa hatutakopa pesa zaidi. Tunapasa kushughulikia na tatizo hili moja kwa moja na tusilipuuze kwani huenda Wakenya ndio wataumia,” Bw Yatani akasema.
Alikariri kuwa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 iliyopitishwa ba bunge la kitaifa Julai 2019 haiwezi kutekelezwa wakati huu kwa kuwa inakabiliwa na changamoto nyingi.
Hata hivyo, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula alitofautia na Bw Yatani akisema ikiwa seneti inaunga mkono mtindo wa serikali wa kukopa pesa nyingi, vizazi vijavyo vitabebeshwa mzigo mzito wa kulipa madeni.
“Serikali ya Jubilee haifai kuruhusiwa kuvizonga vizazi vijavyo na mzigo wa kulipia madeni ambayo hayakufaidi taifa bali sehemu kubwa iliibwa na viongozi mafisadi katika utawala wake,” akasema Bw Wetang’ula ambaye ni kiongozi wa Ford Kenya.
“Haki yako ya kukopa sharti iwe sawa na uwezo wako wa kulipa. Mzigo huo wa kukopa unapaswa kubebwa kwa pamoja na kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” akamwambia Bw Yatani.
Bw Wetang’ula akaongeza: “Serikali haipasi kusisitiza kuwa itaendelea kukopa kiasi cha fedha ambazo haiwezi kulipa.”
Kwa upande wake, Seneta wa Mukueni Mutula Kilonzo Junior alisema hajaridhishwa na sababu ambazo serikali ilitoa kutaka iruhusiwe kuongeza kiwango cha mkopo hadi Sh9 trilioni.
“Unapasa kutushawishi. Kwa sasa sijashawishika na sababu ulizotoa. Mbona unataka kukopa Sh3 trilini zaidi? Haiwezi kuomba idhini yetu bila kutupa sababu zenye mantiki, Bw Waziri. Haupaswi kufanya hivyo!” akafoka Bw Kilonzo Junior.
Akijeteta Bw Yatani alisema mabunge yote mawili yana usemi kwa sababu ndio yataidhinisha mikopo yote, hata kama kiwango cha deni kitaongezeka.
“Mikopo sio mibaya, mradi isimamiwe vizuri na mradi uchumi uweze kumudu viwango vyake,” akaeleza.