Makala

TAHARIRI: Sekta ya michezo katika hali mahututi

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

KWA hakika sekta ya michezo nchini inazidi kudorora. Uozo uliomo umeitumbukiza katika hali mahututi.

Mageuzi ya dharura yanahitajika haraka upesi.

Visa vya usimamizi mbaya wa mashirika, maandalizi duni kwa mashindano ya kimataifa, na wizi wa sare na tiketi za wachezaji si jambo geni.

Uozo wa hivi punde ulifichuka katika kikao cha Kamati ya Bunge kuhusu Michezo ilipobainika kuwa, mabilioni ya pesa zilizotengewa ujenzi wa viwanja saba vya michezo zimetumika vibaya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, shirika la Sport Kenya, ambalo ndilo msimamizi wa fedha za ujenzi huo, lilitoa kandarasi kwa kampuni ambazo zilifanya kazi hewa.

Inahofiwa takriban Sh1.6 bilioni za ukarabati ziliishia mifukoni mwa watu fulani ilhali kazi iliyofanyika ni duni mno.

Kisa kimoja cha kushangaza ni kampuni moja kulipwa Sh132 milioni kufyeka tu nyasi katika uwanja wa Marsabit. Hii ikizingatiwa kwamba shughuli nzima ya ukarabati imetengewa Sh295 milioni.

Iwapo kazi rahisi ya kufyeka nyasi inamenya nusu bajeti, ni bayana kwamba fedha zilizosalia hazitatosha kujenga maeneo ya kuchezea soka na riadha.

Hata uwanja wa kitaifa wa Nyayo katikati mwa jiji kuu la Nairobi umesazwa katika uozo huu.

Tangu kufungwa 2017 ili kufanyiwa ukarabati kazi ni mwendo wa kinyonga licha ya kutumia zaidi ya nusu bilioni. Kulingana na ripoti iliyowasilishwa kwa Kamati ya Bunge, uwanja huo utahitaji zaidi ya Sh612 milioni kukamilika.

Je, bajeti ya ziada kukamilisha ujenzi wa viwanja hivi itatoka wapi?

Ujenzi wa viwanja vya michezo kwa kiwango cha kimataifa katika kaunti zote 47 nchini, ilikuwa ahadi kuu ya serikali ya Jubilee wakati wa kampeni za 2012.

Karibu mwongo mmoja baadaye, hamna uwanja wowote umefikia hata nusu.

Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Amina Mohamed wanafaa kuvalia njuga suala hili.

Waunde jopo kazi maalum na huru litakalotoa mapendekezo ya mageuzi yanayohitajika katika spoti.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ifuatilie waliofyonza fedha za ujenzi ili watupwe jela.

Michezo ndiyo fani pekee iliyosalia kwa vijana kukuza talanta zao na kujitafutia riziki, ikizingatiwa nafasi za kazi zilivyo finyu nchini.