• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
KURUNZI YA PWANI: Kilio cha wataalamu wa kutengeneza maboti Lamu

KURUNZI YA PWANI: Kilio cha wataalamu wa kutengeneza maboti Lamu

Na KALUME KAZUNGU

MAFUNDI wa kutengeneza maboti na mashua katika maeneo mengi ya kaunti ya Lamu wamelalamikia ukosefu wa vifaa muhimu na vya kisasa, hali inayowazuia kupanua biashara hiyo.

Katika mahojiano na Taifa Leo katika visiwa vya Faza, Kizingitini, Kiwayu, Mkokoni, Kiunga, Pate na Siyu, mafundi hao walisema wanakumbwa na wakati mgumu kazini kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kutekelezea kazi zao.

Wanasema wamekuwa wakitumia vifaa wanavyoviona kwa kiasi fulani haviendani na wakati wa sasa kama vile randa, tezo, tindo, patasi, misumeno ya mkono na vifaa vingine vya zamani kutekelezea shughuli zao.

Msemaji wa mafundi hao, Bw Ali Ahmed aliitaka serikali kuwafadhili kwa vifaa vya kisasa vinavyotumia stima ili kutekelezea shughuli zao kwa njia bora na ya haraka zaidi.

Mafundi wa kutengeneza maboti eneo la Faza wakiongozwa na Bw Ali Ahmed (kati) wakilalamikia ukosefu wa vifaa vya kisasa. Wanaomba kufadhiliwa kupata vifaa vya kisasa. Picha/ Kalume Kazungu

Wanasema licha ya biashara ya kutengeneza maboti na mashua kuwa tegemeo kwa familia nyingi Lamu, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa bado hazijatambua sekta hiyo wala kuwajibika kivyovyote katika kuwasaidia wakazi wenye ujuzi wa kutengeneza maboti, mashua na jahazi katika kuboresha ujuzi wao.

Bw Ahmed amemuomba Waziri wa Biashara na Viwanda, Bw Peter Munya, kuzuru Lamu kutathmini maisha magumu ya mafundi hao ili awasaidie kupata fedha, ikiwemo mikopo ili kuwawezesha kupanua sekta hiyo ya ufundi wa maboti.

Mafundi hao wanasema wanaamini iwapo watapata vifaa vya kisasa, muda wanaotumia kutengeneza maboti, mashua au jahazi utafupika.

“Sisi mafundi wa kutengeneza vyombo vinavyotumika katika bahari yetu hapa Lamu, ikiwemo maboti, mashua na jahazi tuko na tatizo kubwa. Bado tunatumia misumeno ya zamani, chapasi, tezo, nyundo na vifaa vingine vilivyopitwa na wakati. Tunaiomba serikali, kupitia Waziri wa Biashara na Viwanda, Peter Munya kutusaidia kupata fedha za kununulia vifaa vya kisasa hata kama ni mikopo. Kwa sasa hutumia kati ya miezi sita na mwaka mmoja kukamilisha boti, mashua au jahazi moja. Iwapo tutapata vifaa vya kisasa, muda tunaotumia kutengeneza vyombo hivi utafupishwa, hivyo kupanua biashara yetu,” akasema Bw Ali.

Bw Lali Shali ambaye ni mmoja wa watengenezaji maboti mashuhuri eneo la Lamu, alisema baadhi ya mafundi wamelazimika kuacha kazi hiyo kufuatia kukosekana kwa miundomsingi mwafaka ya kutekelezea shughuli zao.

Bw Lali Shali akiwa kazini akitengeneza boti lake kwenye ufuo wa Wiyoni mjini Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Shali alisema ni vyema ikiwa kaunti itatenga fedha maalum katika bajeti yake kila mwaka ili kuwasaidia mafundi na wadau wengine katika sekta ya usafiri wa majini kupanua shughuli zao.

“Idadi kubwa ya mafundi wa zamani wamelazimika kuacha kazi kwa kukosa vifaa vya kutekelezea shughuli hiyo. Kaunti ifikirie kutenga fedha ili kusaidia sisi mafundi wa maboti kupata vifaa na pia mafunzo maalumu ya kuongeza ujuzi wetu,” akasema Bw Shali.

Naye Bw Hassan Ramadhan alisema ipo haja ya serikali kufikiria kuwatafutia watengenezaji maboti, mashua na jahazi kaunti ya Lamu soko maalumu la kuuza vyombo vyao punde wanapokamilisha kuviunda.

Bw Ramadhan alisema baadhi ya watu wamekuwa wakiwanunulia mafundi hao vyombo vyao kwa bei rahisi, hatua ambayo anasema inawaumiza.

Kaunti ya Lamu ina watengenezajio maboti, mashua na jahazi zaidi ya 2,000 ambao wote hutegemea mbinu za zamani katika kutekeleza shughuli zao.

You can share this post!

Elachi aongoza sherehe ya kuapishwa kwa wanachama wapya wa...

Wafadhili wahepa Kenya

adminleo