Habari Mseto

Mafuriko yaua watu 29, maelfu wakipoteza makao

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

WATU 29 wamefariki na wengine sita kujeruhiwa, huku mvua iliyopitiliza kiwango inayonyesha ikiendelea kuvuruga hali nchini na kuwaacha maelfu ya watu bila makao na mamia ya mifugo kusombwa na maji.

Akizungumza na vyombo vya habari Alhamisi, Msemaji wa Serikali, Kanali Mstaafu Cyrus Oguna, alieleza kuwa serikali kuu na ile ya kaunti zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kusaidia jamii zilizoathiriwa.

“Kufikia leo (Alhamisi), watu kadha wameathiriwa. Watu 11,700 wamefurushwa makwao. Mifugo 10,000 pia imesombwa na maji. Kufikia sasa pia watu 29 wamefariki na wengine sita wamejeruhiwa,” alisema Bw Oguna akieleza kuwa mashamba mbalimbali yamegubikwa na mafuriko hivyo kuzuia aina yoyote ya kilimo.

Kulingana na Bw Oguna, jumla ya kaunti 25 zilikuwa zimeathiriwa huku kaunti nane miongoni mwake zikiwa zimeathirika vibaya.

Miongoni mwa kaunti zilizo katika hali mbaya zaidi kutokana na mafuriko ni pamoja na: Mandera, Wajir, Marsabit, Turkana, Garissa, Lamu na Kwale.

Msemaji huyo wa serikali pia alieleza kuwa sekta kadha nchini zilikuwa zimeathiriwa ikiwemo sekta ya barabara, elimu, kilimo na maji.

“Serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha sekta hizo zote zimerejeshwa katika njia itakayoboresha maisha ya jamii zilizoathiriwa,” alisema.

Ushirikiano

Alifafanua kuwa serikali ilikuwa ikishirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile Shirika la Msalaba Mwekundu ili kuwasaidia wahasiriwa kupitia mikakati ya muda mfupi na mikakati ya muda mrefu.

“Mikakati ya muda mrefu ni pamoja na vituo vya kuwahifadhi wahasiriwa waliozuiliwa na maji, kusambaza bidhaa za chakula kwa wahasiriwa, usambazaji wa bidhaa zisizo za chakula kama vile blanketi, sodo, sabuni na vyombo vya jikoni,” alisema.

Aliongeza, “Maji na masuala ya usafi pia yameshughulikiwa ikiwemo kuwahamisha walio katika maeneo yaliyofurika kuhamia maeneo ya juu, matibabu kuzuia mkurupuko wa maradhi pamoja na makao ya muda. Usambazaji wa bidhaa zisizo za chakula utaanza leo ambapo bidhaa 500 zitasafirishwa kupitia barabarani kuanzia Nairobi-Isiolo na kisha kusafirishwa kwa ndege hadi Moyale.”

Kuhusu changamoto zinazokabili wakulima wa majani chai, Bw Oguna alisema serikali inajitahidi vilivyo kusaidia wakulima kupata bei inayofaa.