• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya sifa bora za vipenzi wa Mwenyezi Mungu Azzawajalla

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya sifa bora za vipenzi wa Mwenyezi Mungu Azzawajalla

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mungu Azzawajalla, Mola wa walimwengu wetu.

Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam, maswahaba zake kiram na watangu wema siku ya Kiyaamah. Hizi tu ni baadhi ya sifa za wacha Mungu.

Kujiepusha na chuki

Chuki na uadui ni kazi ya shetani. Penye chuki na uadui hapana jema lolote linalofanyika na ni furaha kwa shetani. Chuki inayoruhusiwa kwa Waislamu ni ile ya kuchukia uovu na maadui wa Allah (s.w.) – maadui wa Uislamu na Waislamu.

Waislamu wanakatazwa kuwa na urafiki na maadui wa Allah.

Enyi mlioamini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki, mnaowapelekea (habari zenu) kwa ajili ya urafiki hali yakuwa wameishaikanusha haki iliyokujieni…” (60:1).

Enyi mlioamoni! Msifanye urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia; na wamekata tamaa ya kupata malipo ya Akhera kama walivyokata tamaa makafiri walio makaburini… (60:13).

Enyi mloamoni! Msifanye urafiki na wale walioifanyia mzaha na mchezo dini yenu miongoni mwa wale waliopewa kitabu kabla yenu na miongoni mwa makafiri. Na mcheni Mwenyezi Mungu kama nyinyi na wenye kuamini. (5:57).

Pamoja na hivyo haina maana Waislamu wasiwafanyie uadilifu hawa maadui wa Allah na maadui wa Uislamu, bali Waislamu wataendelea kuwatendea wema na kuishi nao kwa wema iwapo watataka amani.

Kuwa mwenye kusamehe

Mwislamu anatakiwa ajenge tabia ya kuwavumilia wengine. Awe na tabia ya kujihesabu. Ajione kuwa naye kama binaadamu wenzake ni mkosaji na angependa asamehewe na wale aliowakosea kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Kitendo cha kuwasemehe wale waliokukosea ni kitendo cha uchaji Mungu chenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.) Kama inavyobainishwa katika aya zifuatazo:

Na yaendeeni upesi upesi maghufira ya Mola wenu na Pepo (yake) ambaye upana wake (tu) ni (sawa na) mbingu na ardhi. (Pepo) iliyowekewa wamchao Mungu. Ambao hutoa katika (hali ya) wasaa na katika (hali ya) dhiki, na wazuiyao ghadhabu na wanasamehe watu (na wawafanyiao ihsani); na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao hisani. (3:133-134).

Kujizuia na hasira

Kujizujia na hasira ni tabia njema inayoambatana na tabia ya kusamehe. Hasira humpata mtu anapooudhiwa. Wakati mwingine huja ghafla na kumnyima mtu wakati wa kufikiri. Hasira zinaongozwa na shetani, hivyo humnyima mtu nafasi ya kutumia akili, hekima na busara. Hivyo humpelekea mtu kufanya matendo ambayo hugeuka kuwa majuto baadaye. Hasira hasara.

Kujizuilia na hasira ni kitendo cha ucha Mungu chenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.). Rejea Qur’an (3:133-134) na (42:36-37).

Kuwa na subira na uvumilivu

Subira ni kitendo cha kuwa na uvumilivu na utulivu baada ya kupatwa na matatizo au misuko suko mbali mbali katika maisha ya kila siku. Muislamu anatakiwa awe ni mwenye kusubiri baada ya kupata shida au matatizo kama tunavyoamrishwa katika Qur’an.

“Enyi mlioamini! Jisaidieni (katika mambo yenu) kwa kusubiri na kuswali. Bila shaka Allah yupo pamoja na wanaosubiri.” (2:153).

“Enyi mlioamini! Subirini na washindeni wengine wote kwa kusubiri na kuweni imara na mcheni allah mpate kufaulu”. (3:200).

Kufanya subira si jambo jepesi bali ni jambo linalohitaji jitihada na uzima kubwa kama Qur’an inavyoatuusia:

Ewe Mwanangu! Simamisha swala, na uamrishe mema, na ukataze mabaya, na usubiri juu ya yale yatakayokusibu (kwani mwenye kuamrisha mema na kukataza mabaya lazima zitamfika tu taabu); Hakika hayo ni katika mambo yanayostahiki kuazimiwa (na kila mtu). (31:17).

Kuwa mkarimu

Ukarimu ni miongoni mwa tabia njema anayotakiwa ajipambe nayo Muislamu. Muislamu anatakiwa awe mwepesi wa kuwakirimu wengine kwa kuwasaidia wakati wanapokuwa katika hali ya kuhitajia msaada bila ya kutarajia malipo yoyote kutoka kwao. Sifa ya wakarimu inabainishwa katika aya zifuatazo:

Na huwalisha chakula maskini na mayatima na wafungwa, na hali yakuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho). (Husema wenyewe katika nyoyo zao wanapowapa chakula hicho): “Tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu (tu) hatutaki kwenu malipo wala shukrani”. “Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu”. (76:8-10).

Kujiepusha na uchoyo na ubahili

Uchoyo na ubahili ni kinyume cha ukarimu. Mtu mchoyo ana kasoro katika imani yake. Anaona kuwa chochote alichonacho amekipata kwa jitihada na akili yake tu. Pia anahofu kuwa akitoa kumpa mwingine atapungukiwa au atafilisika. Mtume (s.a.w.) Ametunabahisha hilo katika hadithi zifuatazo:

Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Mtu anasema: “Hiki changu! Hiki changu! Lakini ukweli ulivyo ni kwamba, vilivyo vyake katika mali yake ni vitu vitatu: “Kile alichokula au kile alichokitoa sadaqa (hakika) amekiweka akiba, na kingine chochote zaidi ya hivi, hakika si vyake (si vyenye kumfaa) na ataondoka awaachie watu”. (Muslim).

Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: “Chakula cha watu wawili kina watosha watu watatu, na chakula cha watu watatu kinawatosha watu wanne”. (Bukhari na Muslim).

Kuwa mwenye kutosheka

Kutosheka ni kuridhika na neema uliyonayo. Kutosheka ni utajiri kuliko utajiri wote uliopo ulimwenguni.

Abu Hurairah (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema, utajiri si kuwa na mali nyingi lakini utajiri ni kutosheka”. (Bukhari na Muslim).

Muislamu anatakiwa awe ni mwenye kutosheka na kile alichoruzukiwa na Mola wake.

Kila mtu amekadiriwa riziki yake na Allah (s.w.). Hakuna mwenye uwezo wa kumpunguzia au kumzidishia mtu riziki. Hili linabainishwa katika Qur’an katika usia wa Mzee Luqman kwa wanawe:

Ewe mwanangu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi, Mwenyezi Mungu analileta (amlipe aliyefanya); bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo yaliyofichikana, (na) Mjuzi wa mambo yaliyo dhahiri. (31:16).

Kujiepusha na husuda

Husuda ni miongoni mwa magonjwa makubwa ya moyo. Mtu mwenye husuda anadonda la chuki moyoni mwake, juu ya neema alizoneemeshwa mwingine na Mwenyezi Mungu (s.w.). Kwa maana nyingine anachukia utaratibu wa Mwenyezi Mungu (s.w.) aliouweka katika kugawanya neema zake kwa waja wake. Hasidi kutokana na chuki yake dhidi ya mja aliyeneemeshwa na Mwenyezi Mungu (s.w.), huwa tayari kwa hali na mali kumdhuru mja huyo asiye na hatia yoyote. Ni kwa msingi huu Mwenyezi Mungu (s.w.) Anatufundisha kujikinga kwake na shari za viumbe vyake, akiwepo hasidi kama tunavyosoma katika Suratul-Falaq:

Sema: “Ninajikinga na Mola wa Ulimwengu wote na shari ya Alivyoviumba, na shari ya giza la usiku liingiapo na shari ya wale wanaopulizia mafundoni na shari ya hasidi anapohusudu:. (113:1-5).

Kuwa wenye msimamo thabiti (Istiqama)

Muumini wa kweli anayemtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.) Kwa kila hali hana budi kuwa na msimamo thabiti katika kuusimamisha na kuufuata Uislamu.

Si muumini wa kweli yule anaeyumbayumba (mudhadhabina) kwa kuchanganya haki na batili au utii na uasi katika kuendesha maisha yake ya kila siku. Mwenyezi Mungu (s.w.) Ametuamrisha wale tutoao shahada ya kweli tuingie Uislamu wote au tuwe Waislamu katika kila kipengele na kila hatua yetu ya maisha na wala tusiingie nusu nusu. Anatuamrisha: Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu wote, wala msifuate nyayo za shetani, kwa hakika yeye kwenu ni adui dhahiri. (2:208).

You can share this post!

AIBU KUU: Origi abaguliwa kwao nchini Ubelgiji

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mwislamu anavyopaswa kujiandaa na...

adminleo