• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
MWANAMKE MWELEDI: Jina lake hutikisa wanariadha duniani

MWANAMKE MWELEDI: Jina lake hutikisa wanariadha duniani

Na KEYB

JINA lake linapotajwa, ulimwengu wa riadha humu nchini na kimataifa sharti umvulie kofia. Sio mwingine bali ni Vivian Jepkemoi Cheruiyot, mmojawapo wa wanariadha wa kike wanaoheshimika sana kutoka humu nchini.

Kwa takriban miongo miwili, mwanariadha huyu amekuwa malkia kwenye mbio za mita 3,000, 5,000, 10,000, na hata marathon, na katika harakati hizo kujishindia nishani kwenye mbio za kitaifa na kimataifa.

Lakini ni katika mbio za mita 5,000 ambapo Bi Cheruiyot ameng’aa na kuwa tishio kwa wanariadha hasa wa Ethiopia ambao kwa miaka wametawala mbio hizi.

Ni suala alilothibitisha mwaka wa 2016 kwenye michezo ya Olimpiki jijini Rio de Janeiro Brazil, alipotwaa nishani ya dhahabu kwenye mbio hizo, na hata kuvunja rekodi ya mashindano hayo. Pia, hapa aliandikisha vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa Mkenya wa kwanza wa kike kushinda taji hilo. Aidha, alishiriki katika mbio za mita 10,000 na kushinda nishani ya fedha.

Anajivunia kuiwakilisha Kenya kwenye mbio za Olimpiki mara tatu. Alishiriki kwenye michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza mwaka wa 2008 jijini Beijing, China.

Mwaka wa 2012 pia alishiriki kwenye michezo ya Olimpiki iliyoandaliwa jijini London, Uingereza, ambapo alitwaa nishani ya fedha katika mbio za mita 5,000, na ya shaba kwenye mbio za mita 10,000.

Aidha, ameshiriki katika mbio zingine humu nchini na kimataifa kama vile mashindano ya IAAF, mbio za marathon na hata michezo ya madola, na katika harakati hizo kujishindia nishani kochokocho.

Mwaka wa 2018 alishinda London Marathon nchini Uingereza. Mwaka huo huo alimaliza wa pili kwenye New York Marathon, nyuma ya mshindi, Mary Keitany.

Aidha, anashikilia rekodi ya kitaifa katika mashindano ya madola, kwenye mbio za mita 10,000.

Ufanisi huu umemfanya kutambuliwa sio tu humu nchini, bali pia katika ngazi za kimataifa. Mwaka wa 2012, alipewa tuzo ya Laureus Female Athlete of the Year, mwanariadha wa kike wa mwaka kwa mujibu wa jarida la riadha la Track and Field Magazine, nchini Amerika.

Aidha, Bi Cheruiyot alitambuliwa kama mmojawapo wa wanaspoti mahiri wa kike kwa mujibu wa Laureus World Sports Academy, na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza Mkenya, na raia wa pili wa Kenya kutambuliwa kwenye jukwaa hili.

Sio hayo tu, mwaka wa 2009, alipewa tuzo ya ‘The State Order of the Grand Warrior (OGW)’ baada ya kutwaa nishani ya dhahabu kwenye mbio za mita 5,000 katika michezo ya Olimpiki, jijini Beijing.

Mzaliwa wa eneo la Kerio, kama watoto wengi eneo la bonde la ufa, ndoto yake kwenye riadha ilichongwa kwa kutazama baadhi ya magwiji kutoka sehemu hiyo.

Alianza kukimbia akiwa bado mdogo huku ari yake ikichangiwa hasa na mwanariadha Alice Timbilili kwani walikuwa wanatoka katika kijiji kimoja.

Nyota yake katika ulimwengu wa riadha ilianza kung’aa mwaka wa 1999, akiwa na umri wa miaka 15 pekee, alipomaliza wa pili na kutwaa nishani ya fedha katika mbio za IAAF World Cross-Country Championships.

Mwaka huo huo katika mashindano ya riadha ya ulimwengu kwa vijana – World Youth Championships, alishinda nishani ya shaba kwenye mbio za mita 3,000.

Ni hapa alipopata mwaliko kwenye kikosi cha watu wazima ili kushiriki kwenye mbio za All-Africa Games, ambapo alijinyakulia nishani ya shaba katika mbio za mita 5,000.

Huku Kenya ikizidi kutambuliwa kama taifa lililojaa vipaji katika riadha, Bi Cheruiyot kwa upande wake ametia bidii na kuhakikisha kwamba jina lake linaorodheshwa miongoni mwa magwiji wa fani hii.

You can share this post!

UMBEA: Hata kama ni dhahiri kosa si lako, omba msamaha...

Safaricom ‘iliwekewa presha’ kuteua Mkenya

adminleo