USHINDI WA TABU: Manchester United, Arsenal wapeleka mahangaiko Europa
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
KLABU za Arsenal, Manchester United na Wolves zilizoa ushindi muhimu japo kwa jasho Jumatano kwenye Ligi ya Europa dhidi ya Vitoria, Partizan Belgrade na Slovan Bratislava, mtawalia.
Arsenal ya kocha Unai Emery ilihitaji mabao mawili katika dakika za lala-salama kutoka kwa mchezaji wake ghali kabisa Nicolas Pepe kulemea Vitoria 3-2 uwanjani Emirates.
United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ilichabanga Partizan Belgrade 1-0 kupitia penalti ya Anthony Martial nchini Serbia nayo Wolves ilichapa Slovan Bratislava 2-1 nchini Slovakia katika mechi ambayo Diogo Jota alilishwa kadi nyekundu.
Pepe alitoka kwenye benchi na kuona lango mara mbili. Ushindi huu ulipatia utulivu kocha Unai Emery, ambaye amejipata akikosolewa.
Baada ya kunyukwa 1-0 na Sheffield United kwenye Ligi Kuu mnamo Jumatatu, Emery alilazimika kujitetea vikali kabla ya kukutana na Vitoria katika mechi ya Kundi F.
Kilichofuata kichapo hicho ni mchezo mwingine duni ambao Arsenal iliponea baada ya Pepe kuona lango dakika ya 80 na dakika ya pili ya majeruhi. Pepe alinunuliwa kwa Sh9.5 bilioni kutoka Lille mwezi Agosti.
Bila bao katika mechi mbili za kwanza na pia kukosa ushindi barani Ulaya tangu mwaka 2005, Vitoria iliduwaza uwanjani Emirates ilipochukua uongozi kupitia kwa winga wa zamani wa Tottenham, Marcus Edwards dakika ya nane.
Bruno Duarte alirejesha Vitoria mbele baada ya Gabriel Martinelli kusawazisha 1-1 na timu hiyo kutoka Ureno ililinda ngome yake vyema hadi dakika 10 za mwisho iliposambarika.
Kukiwa na bango zaidi ya moja uwanjani lenye maandishi “Emery Out” na pia mashabiki kuimbia wimbo Mesut Ozil, ambaye tena alikuwa nje ya kikosi, inaonekana ombi la Emery la kutaka wawe na subira halikuwashawishi.