Watoa hisia mseto kuhusiana na BBI
Na SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA
WANDANI wa Naibu Rais William Ruto kutoka Magharibi mwa Kenya, wameahidi kuunga mkono, japo shingo upande, ripoti ya Jopokazi la maridhiano (BBI) ambayo inatarajiwa kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Lakini katika Kaunti ya Kitui zaidi ya wabunge 10 wanawake wanachama wa vuguvugu la “The Embrace” waliahidi kuunga mkono kwa dhati ripoti hiyo wakisema mapendekezo yake yataleta amani na uthabiti nchini.
Wabunge kutoka Bungoma, Busia na Kakamega walioandamana na Dkt Ruto alipoongoza hafla ya uzinduzi wa Chuo cha Kiufundi cha Wanga, Mumias, walisema wataunga mkono ripoti ikiwa itapendekeza uwepo wa usawa katika usambazaji wa rasilimali ya kitaifa na kuongezwa kwa fedha katika kaunti.
Lakini wabunge hao, Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), John Waluke (Sirisia), Enock Kibunguchy (Likuyani) na Geofrey Omuse (Teso Kusini) na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale walisema wataipuuza ripoti hiyo ikiwa itapendekeza kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za utawala.
“Aidha, tutapinga ripoti hiyo ikiwa itawapokonya wananchi haki ya kuchagua Rais wao moja kwa moja katika uchaguzi mkuu na kuwatwika wabunge jukumu hilo,” akasema Bw Washiali.
Hata hivyo, Mbunge huyo ambaye ni kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa alisema ripoti ya BBI ingali uvumi kwani haijawasilishwa rasmi kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Naye Dkt Khalwale alisema Wakenya hawaelewi ni kwa nini wanachama wa jopo la BBI walibuni wazo kwamba Rais achaguliwe katika bunge.
Hata hivyo, aliahidi kuongoza kampeni ya kitaifa ya kuwawezesha Wakenya kuelewa yaliyomo katika ripoti hiyo baada ya kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Ruto akwepa
Lakini kuwa upande wake Dkt Ruto alikwepa kuzungumzia suala la BBI na kuangazia umuhimu wa elimu ya kiufundi katika kusukuma ajenda ya serikali ya ustawi wa kiviwanda.
Kuhusu kampuni ya Sukari ya Mumias, Dkt Ruto alisema serikali imekuwa ikitenga mabilioni ya fedha kufadhili mpango wa kuufufua lakini faida ya fedha hizo haijaonekana kutokana na usimamizi mbaya.
Na katika kaunti ya kundi la The Embrace, likiongozwa na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi waliapa kuendesha kampeni ya kuwahamasisha Wakenya kuhusu yaliyomo katika ripoti ya BBI.