Wizara yajitenga na madai ya kugundulika alikozikwa Dedan Kimathi
Na CHARLES WASONGA na MARY WANGARI
SERIKALI imepuuzilia mbali ripoti kwamba kaburi la mpiganiaji uhuru Shujaa Dedan Kimathi limepatikana katika gereza la Kamiti.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumamosi wizara ya masuala ya ndani ilisema habari kama hizo sharti zipitishwe na mikondo rasmi ya mawasiliano ya serikali wala sio njia nyinginezo.
“Tunarejelea habari zinazosambazwa katika majukwaa mbalimbali ya habari kwamba kaburi la mpiganiaji uhuru Shujaa Dedan Kimathi imepatikana katika magereza ya Kamiti. Izingatiwe kuwa madai hayo ni ya uwongo,” wizara hiyo inayoongozwa na Fred Matiang’i ikasema kupitia ukurasa wake wa akaunti yake ya mtandao wa Twitter.
Mnamo Ijumaa, Oktoba 25, 2019, mashirika mengi ya habari yalisambaza habari hizo, hatua ambayo ilisemekana kuwa mwisho wa juhudi za kusaka kaburi hiyo ambazo zimeendelea kwa miongo kadha.
Msimamo wa serikali unamaanisha nini?
Wapo sasa wanaohisi pengine serikali inachelea kukubali hilo kwa sababu yapo makundi yatakayojizolea umaarufu.
Habari hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Wakfu wa Dedan Kimathi Evelyn Wanjugu Kimathi ambaye ni bintiye Shujaa huyo aliyeuawa na wanajeshi wa serikali ya ukoloni miaka 66 iliyopita.
“Ni kwa furaha kuu tunatangaza kuwa baada ya juhudi nyingi za pamoja zilizoongozwa na Serikali ya Jamhuri ya Kenya, eneo la kaburi la shujaa wa uhuru Field Marshall Dedan Kimathi Waciuri hatimaye limetambuliwa. Eneo hilo ambalo limekuwa likisakwa kwa miaka mingi, liko katika jela ya Kamiti Maximum,” ilisema familia hiyo kupitia taarifa kutoka kwa Wakfu wa Dedan Kimathi iliyotolewa mnamo Ijumaa.
Bintiye shujaa huyo Bi Evelyn Wanjugu Kimathi, ambaye pia ndiye mkurugenzi wa Wakfu wa Dedan Kimathi alisema familia hiyo sasa ilikuwa ikisubiri kwa hamu kibali kutoka kwa Jaji Mkuu David Maraga, iki kuweza kufukua mabaki ya babake na kumpa mazishi ya heshima.
Aidha, alisema ufanisi huo ulikuwa habari kuu sio tu kwa familia ya shujaa Kimathi bali vilevile kwa jamii ya mashujaa wa kupigania uhuru, huku akiwashukuru wote waliohusika kufanikisha juhudi hizo.
Wanjugu alisema kuwa sasa wanasubiri amri kutoka kwa Jaji Mkuu David Maraga kabla ya kufukuliwa kwa mifupa ya Kimathi kwa ajili ya kupewa mazishi ya heshima na taadhima.
Shujaa Kimathi alifariki mnamo Februari 1957 akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuhukumiwa na kunyongwa kwa makosa ya mauaji na ugaidi na serikali ya ukoloni wa Mwingereza.
Alikuwa ni kiongozi wa walioasi serikali ya kikoloni, ambayo ilimtaja kama gaidi, pamoja na wenzake waliopinga utawala huo.
Serikali ya Rais mstaafu Mwai Kibaki ilimtawaza Kimathi kuwa Shujaa mnamo 2007 wakati wa ukumbusho wa kifo chake. Sanamu yake ilizinduliwa kama kumbukumbu ya juhudi zake za kupigania uhuru wa taifa hili. Sanamu hiyo iko kwenye makutano ya barabara ya Kimathi na ile ya Mama Ngina, katikati mwa jiji la Nairobi.