Mvua yatarajiwa kwingi mtihani wa KCPE ukianza
Na WAANDISHI WETU
MVUA inatarajiwa leo Jumatatu asubuhi katika maeneo mengi ya nchi wakati watahiniwa wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) watakapofanya maandalizi ya mtihani huo.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa jana ilisema mvua itanyesha asubuhi katika maeneo ya Pwani, Mashariki, Magharibi, Kati na sehemu chache Kaskazini Mashariki ya nchi.
Katika Kaunti ya Kitui, wanafunzi kutoka zaidi ya shule 30 za msingi na upili zinazopatikana eneobunge la Mwingi ya Kati watakabiliwa na hali ngumu kufika shuleni baada ya daraja la pekee la Mto Enziu kuporomoka kutoka na mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa eneo hilo.
Daraja hilo ambalo miaka ya nyuma limesababisha vifo vya raia lilisombwa na maji ya mvua mnamo Alhamisi huku mamia ya wasafiri waliokuwa wakielekea mji wa Mwingi wakikwama kwenye pande zote mbili za daraja hilo.
“Tuna shule 30 za msingi na upili ambazo zinategemea daraja hili kufika mji wa Mwingi. Serikali italazimika kutumia ndege aina ya helikopta kusafirisha karatasi za mtihani ijapokuwa jamii ya hapa inateseka sana,” akasema mfanyabiashara Peter Mulavu.
Mradi wa ujenzi wa daraja hilo ulianzishwa na aliyekuwa mbunge Joe Mutambu lakini ikatelekezwa na mrithi wake Gideon Mulyungi.
Katika eneo la Bonde la Ufa, matayarisho ya mtihani wa kitaifa wa KCPE nayo yamekamilika ambapo wanafunzi zaidi ya 300,000 wanatarajiwa kufanya mtihani huo.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi wa elimu katika eneo hilo Bw John Ololtuaa kwenye mahojiano na na Taifa Leo.
Bw Ololtuaa alisema kuwa mtihani huo wa KCPE unatarajiwa kufanyika katika vituo zaidi ya 8,000 katika eneo hilo huku kukiwa na wasimamizi zaidi ya 23,000 ambao watakuwa wakiusimamia.
Kati ya watahiniwa hao, kuna pia wafungwa 225 ambao wanatarajiwa kufanya mitihani ya kitaifa. Kati ya wafungwa hao, 208 watafanya mtihani wa wa KCPE ulhali wafungwa 17 watafanya KCSE.
“Kwa ujumla tuko na wafungwa 208 ambao ni watahiniwa katika mtihani wa KCPE na wafungwa 17 ambao ni watahiniwa katika mtihani wa KCSE. Tumeweka mazingira salama ili tuhakikishe kwamba wanafanya mitihani yao bila taabu wala matatizo yoyote,” akasema Bw Ololtuaa.
Katika Kaunti ya Kirinyaga, imebainika kwamba idadi ya wasichana watakaofanya mtihani wa KCPE ni wa juu kuliko wavulana.
Kulingana na Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo Abdikadir Hassan, wasichana 7,127 wataufanya mtihani huo ikilinganishwa na wavulana 6,708.
“Ni ukweli kwamba idadi ya wasichana ambao watakuwa wanafanya mtihani huo ni wa juu kuliko wavulana,” akasema Bw Hassan.
Afisa huyo aliyekuwa akizungumza mjini Kerugoya aliwatakia kila la kheri watahiniwa na akasema kwamba usalama umeimarishwa vilivyo wakati wa KCPE na hata KCSE inayoendelea.
“Tumekutana na maafisa wa ngazi za juu katika idara ya polisi na kuzungumzia masuala ya usalama. Tutahakikisha kwamba hakutokei sababu zozote ambazo zitavuruga mtihani huu,” akasema Bw Hassan.
Alikiri kwamba baadhi ya shule zimeathirika na mafuriko kutokana na mvua lakini akasema hilo kuna magari ya kutosha ya kusafirisha karatasi za mtihani kutoka vituo vinakohifadhiwa hadi shule mbalimbali.
Ripoti za Cecil Odongo, Samuel Baya, George Munene na Kitavi Mutua