DIMBA: Kizibo cha Messi tineja Ansu Fati atisha kweli!
Na CHRIS ADUNGO
ANSSUMANE ‘Ansu’ Fati Vieira, 16, ni winga chipukizi wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania ambaye ni mzaliwa wa Guinea-Bissau.
Kwa pamoja na familia yake, walihamia katika eneo la Herrera viungani mwa mji wa Seville, Uhispania akiwa na umri wa miaka sita pekee. Hii ilikuwa baada ya kakaye mkubwa, Braima kuingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Sevilla. Kakaye mwingine, Miguel pia ni mwanasoka matata ambaye kwa sasa huvalia jezi za akademia ya Barcelona.
Baba yao, Bori Fati ni raia wa Guinea-Bissau ambaye ana usuli nchini Ureno.
Bori alihamia Uhispania na kuajiriwa kuwa dereva mjini Mainaleda baada ya kuwa ombaomba wa barabarani kwa kipindi kirefu jijini Seville.
Fati ambaye alikwezwa ngazi kutoka akademia ya Barcelona kuchezea kikosi cha kwanza msimu huu, aliweka historia Septemba 2019 kwa kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi ugani Camp Nou kuwahi kufunga bao ndani ya jezi za wapambe hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Tineja huyu alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufunga bao chini ya dakika sita za kuletwa ugani katika sare ya 2-2 iliyosajiliwa na Barcelona dhidi ya Osasuna katika kipute cha La Liga. Alijiunga na akademia ya Barcelona almaarufu ‘La Masia’ mnamo 2012.
Kiini cha kocha Ernesto Valverde kumwajibisha Fati katika mchuano wa haiba kubwa dhidi ya Valencia ni ushawishi uliodhihirishwa na kikembe huyu ugani wakati alipokuwa akicheza dhidi ya Osasuna mjini Pamplona.
Fati aliweka historia ya kuwa mchezaji chipukizi zaidi tangu 1941 kuwahi kuchezea Barcelona alipowajibishwa dhidi ya Real Betis mnamo Agosti 25, 2019.
Kuchezeshwa kwake katika msururu wa mechi za baadaye katika La Liga na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kulichochewa pia na jeraha lililokuwa likiuguzwa na nahodha Lionel Messi ambaye alikuwa mwingi wa sifa kwa chipukizi huyo hasa baada ya ushirikiano mkubwa kati yake na sajili mpya Frenkie De Jong kuwatatiza sana mabeki wa vikosi pinzani.
Kulingana na Valverde, Fati ana uwezo wa kumpiku Cristiano Ronaldo wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno na kufikia kiwango cha Messi hivi karibuni.
Kufikia sasa mwishoni mwa mwaka 2018 Fati ambaye kwa sasa kiwango chake kinalinganishwa na cha chipukizi Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Ufaransa, bado hakuwa amechezea taifa lake la Guinea-Bissau.
Ni jambo lililowachochea vinara wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) kumjumuisha katika timu ya taifa ya makinda watakaowania ufalme wa Kombe la Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 baadaye mwaka 2019.
Akiwa na umri wa miaka 16 na siku 304, kwa sasa ndiye sogora wa tatu mwenye umri mdogo zaidi katika La Liga baada ya mvamizi wa zamani wa Malaga Fabrice Olaga (miaka 16 na siku 98) na Iker Muniain wa Athletic Bilbao (miaka 16 na siku 289).
Baada ya kuvalia jezi za Herrera na kuridhisha pakubwa katika kikosi cha chipukizi kambini mwa Sevilla, Fati alisajiliwa na Barcelona mnamo 2012 akiwa na umri wa miaka 10.
Alitia saini mkataba wake wa kwanza kitaaluma mnamo Julai 24, 2019 katika maelewano ambayo kwa sasa yanatarajiwa kumdumisha kambini mwa Barcelona hadi mwishoni mwa 2022.
Bao lake la kwanza ndani ya Barcelona lilitokana na mechi iliyowashuhudia wakilazimishiwa sare ya 2-2 dhidi ya Osasuna mnamo Agosti 31, 2019. Alipangwa katika kikosi cha kwanza dhidi ya Valencia mnamo Septemba 14 ambapo aliweka historia ya kuwa chipukizi wa kwanza katika La Liga kufunga bao na kuchangia jingine akiwa na umri wa miaka 16 na siku 318.
Fati aliwafungia Barcelona bao katika dakika ya pili na kuchangia jingine lililojazwa wavuni na De Jong dakika tano baadaye katika ushindi mnono wa 5-2 waliousajili dhidi ya Valencia mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.
Siku nne baadaye, aliwajibishwa kwa mara ya kwanza katika kivumbi cha UEFA dhidi ya Borussia Dortmund waliowalazimishia sare tasa nchini Ujerumani. Tukio hilo lilimfanya kuivunja rekodi ya Bijan Krkic aliyewahi kuchezeshwa na Barcelona katika UEFA akiwa na umri wa miaka 17 na siku 22 pekee.
Alijumuishwa katika kikosi cha Uhispania cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 mnamo Oktoba 11, 2019 baada ya Carles Perez kupata jeraha. Mchuano wake wa kwanza kunogesha katika ulingo wa kimataifa ni ule uliowakutanisha Uhispania na Montenegro mapema Oktoba.