Habari

IMF yapongeza vita dhidi ya ufisadi na mageuzi ya kiuchumi nchini

October 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Fedha Ulimwenguni (IMF) limeipongeza Kenya katika juhudi zake za kupambana na ufisadi, ikielezea matumaini kuwa nchi hii itashinda vita hivyo.

Mkurugenzi wa shirika hilo anayesimamia Ustawi wa Afrika Abebe Selassie pia alisema wameridhika na kiwango cha ukuaji wa kiuchumi nchini ambacho wakati huu ni kati ya asilimia 5.5 na asilimia 6.0.

Hali hiyo inatokana na mabadiliko ambayo inatekelezwa na serikali katika sekta ya usimamizi wa kifedha nchini.

“Kwa sababu hii, Kenya inaongoza katika nyanja za mageuzi ya kiuchumi na ukuaji katika ukanda wa Afrika Mashariki,” Bw Abebe akasema Jumatatu alipokutana na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Wakati wa mkutano huo, Rais Kenyatta na Bw Abebe walijadili ushirikiano kati ya Kenya na IMF huku kiongozi wa taifa akisema Kenya itaendelea kufanya kazi na shirika hili kwa minajili ya kufanikisha ajenda zake za maendeleo.

Rais Kenya aliipongeza IMF kwa kuipa Kenya kuendelea kuisadia serikali kutekeleza miradi yenye manufaa kwa Wakenya.

Wakati wa mkutano huo, Bw Abebe alimjulisha kwa Rais Kenyatta, Tobias Rasmussen ambaye sasa ndiye atakuwa mwakilishi wa IMF nchini Kenya.

Bw Rasmussen anachukua pahala pa Jan Mikkelsen ambaye kipindi chake cha kuhudumu kilikamilika mnamo Septemba 13, 2019.

Rais Kenyatta aliwahakikishia maafisa hao wa IMF kwamba milango yake iko wazi kwa majadiliano ambayo yanalenga kunufaisha taifa hili.

“Milango yetu iko wazi. Nalenga kufanya kazi nawe kwa karibu,” Rais Kenyatta akamwambia Bw Rasmussen, mwakilishi mpya wa IMF nchini Kenya.

Bw Abebe yuko nchini Kenya kuzindua ripoti ya IMF kuhusu Hali ya Kiuchum katika Mataifa ya Afrika yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara.

Maafisa wa serikali ya Kenya waliohudhuria mkutano huo wa Ikuli ni pamoja na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, Katiba wa Wizara ya Fedha Julius Muia, mshauri wa masuala ya fedha katika Wizara ya Fedha Dkt Geoffrey Mwau miongoni mwa wengine.