• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
TAHARIRI: Tusikubali vurugu zitawale kampeni

TAHARIRI: Tusikubali vurugu zitawale kampeni

Na MHARIRI

VURUGU zilizoshuhudiwa wikendi katika eneobunge la Kibra ni aibu kubwa kwa viongozi wa siasa humu nchini.

Katika kilele cha kampeni za uchaguzi mdogo utakaofanywa Alhamisi wiki ijayo, viongozi wakuu wawili walivamiwa na vijana.

Kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi alivamiwa na vijana waliomrushia mawe. Bw Mudavadi alikuwa ameenda katika uwanja wa Kamukunji eneo la Kibra, kumpigia debe mwaniaji wa chama hicho, Bw Eliud Owalo.

Inasemekana kundi la watu liliandama gari la Bw Mudavadi na kuanza kulirushia mawe, hatua iliyomlazimu kukatiza hotuba yake.

Tukio sawa na hilo lilirejelewa katika uwanja wa Bukhungu huko huko Kibra, wafuasi wa chama cha Ford Kenya walipomshambulia kinara wa ODM, Raila Odinga kwa kusimama kwa muda mahali hapo, ilhali walikuwa wamepata kibali cha kuutumia.

Vijana wa Ford Kenya walidai kuwa Bw Odinga hakupaswa kuhutubu hapo, kwa kuwa eneo hilo lilikuwa la kumfanyia kampeni mgombeaji wao, Mhandisi Khamisi Butichi.

Matukio haya yanaonyesha kutokomaa kwa Wakenya kuhusiana na kampeni za kisiasa. Ni dhahiri kuwa wapigakura wengi hawana habari kuhusu sheria za uchaguzi, ambazo zinakataza vurugu za aina yoyote katika kampeni.

Lengo la wanasiasa kufanya kampeni kabla ya uchaguzi, ni kuuza sera kwa umma ili yule atakayefanikiwa kuwashawishi watu, achaguliwe.

Kuwavamia watu kwa sababu wamesimama katika eneo mnaloamini kuwa ngome ya chama au mwaniaji fulani, sio tu ushenzi, bali dhihirisho kuwa mtu hajakomaa kisiasa.

Bw Odinga na Bw Mudavadi walikuwa na haki kama vinara wa vyama vyao, kuzungumza na wapigakura wote wa Kibra, ili wawaeleze ni kwa nini wanaamini wawaniaji wao ndio bora kuliko wengine.

Katika siasa, muhimu kwa mpiga kura ni kusikiza. Uamuzi wa mwisho huwa debeni, ambapo mpiga kura hujifungia peke yake na kutoa kauli ya mwisho.

Kwa hivyo, japo polisi walichukua hatua na kufyatua vitoa machozi kutawanya vijana hao, kuna haja ya kuchukua hatua zaidi. Idara zinazohusika na nidhamu katika uchaguzi, zina jukumu la kuhakikisha watu wanaelewa umuhimu wa kufanya kampeni kwa njia ya amani. Tusiruhusu wahuni kuingiza vurugu katika kampeni.

You can share this post!

Ajuta kudai kipusa ni ‘slay queen’

Kura ya maamuzi ifanyike 2022, Duale ashikilia

adminleo