Kimataifa

Amerika yakashifu ukatili waliotendewa wanafunzi Makerere

October 29th, 2019 2 min read

Na AFP

KAMPALA, Uganda

UBALOZI wa Amerika nchini Uganda umekashifu vikali ukatili waliotendewa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere na maafisa wa polisi wakati wa mgomo Alhamisi iliyopita huku ukiitaka serikali kuingila kati.

“Ubalozi wa Amerika nchini Uganda umetatizwa mno na dhuluma katika Chuo Kikuu cha Makerere kuhusiana na maandamano yanayoendelea dhidi ya nyongeza za karo zilizopendekezwa. Video za maafisa wa usalama wakiwashambulia wanafunzi ambao hawakuwa wamejihami katika ukumbi wa mikutano pamoja na mashambulizi dhidi ya wanahabari waliokuwa wakifuatilia maandamano hayo, hasa ni ya kutatiza mno,” ilisema taarifa ya Amerika.

Ikaongeza: “Hatua hii kali ya huduma ya ulinzi haifai na ni ukiukaji dhahiri wa haki za kukusanyika, kuzungumza na kujieleza, zinazohakikishwa na katiba ya Uganda. Tunahimiza serikali ya Uganda kuwaruhusu raia wake wote kufurahia haki zao kwa njia ya amani bila hofu.”

Msemaji wa polisi Fred Enanga alitetea matumizi ya nguvu ya kikosi hicho cha pamoja cha maafisa wa usalama katika kusaka ukumbi wa mikutano wa wanafunzi.

“Pindi kamanda wa polisi anapotoa amri wakati wa ghasia akiamrisha mwache kuzua fujo, mnapaswa kutii,” alisema Bw Enanga, akisema kuwa kinachotendeka baadaye hata kama kinahusu kifo, afisa wa polisi hawezi kulaumiwa.Hata hivyo, Sheria ya Polisi inaruhusu tu matumizi ya nguvu ambayo yanaambatana na pingamizi.

Bw Enanga alisema walipokea habari za kijasusi kuhusu kuwepo kwa kikosi cha tatu kilichohusika na ghasia hizo.

Alisema idadi kubwa ya wanafunzi walikuwa wametoa hela zilizotumwa na mtu ambaye hakumtaja na kwamba walizichukua kutoka kwa ajenti mmoja wa kituo cha kutuma hela kupitia rununu chuoni humo.

Uchochezi

Alisema kundi hilo limekuwa likiwachochea wanafunzi kutoka vyuo vikuu vinginevyo kama vile Kyambogo na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Makerere Nakawa kujiunga na maandamano hayo.

Chama cha Forum for Democratic Change (FDC) kimelaani kuhusika kwa jeshi katika mgomo wa wanafunzi na kuitaka serikali kuwaondoa wanajeshi mara moja.

Ibrahim Ssemujju Nganda, msemaji wa chama hicho jana alieleza vyombo vya habari katika makao makuu ya FDC Najjanankumbi kuwa hatua ya kuvunja vyumba vya wanachuo ilikuwa “ugaidi mbaya zaidi na udhalilishaji ambao kiongozi yeyote anaweza kutendea watu wake.”