Makala

GWIJI WA WIKI: Philip Opetuh

October 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

JITOLEE kwa hali na mali kufanya kazi uliyopewa ili ubora wako katika utekelezaji wa majukumu hayo uwe msingi wa sifa utakazopokezwa na wenzako au waajiri wako.

Baada ya kuiwasha taa yako ya mafanikio, usiifiche mvunguni. Badala yake, pania sana kuiweka katika sehemu za juu ili kila mtu afaidike kutokana na mwangaza wake.

Kabla ya kufanya maamuzi yoyote, taka sana kutathmini kwa kina athari za uteuzi huo ili hatimaye usijipate katika ulazima wa kujutia nyingi za hatua ulizozichukua maishani. Hakuna siri zaidi iliyo na uwezo wa kukufanikisha katika chochote unachokifanya isipokuwa bidii, ustahimilivu, nidhamu na kumcha Mungu.

Huu ndio ushauri wa Bw Philip Opetuh, mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Msingi ya PEFA Donholm, Nairobi.

Maisha ya awali

Opetuh alizaliwa mnamo Mei 9, 1986, katika kijiji cha Lukongo, eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega akiwa mtoto wa tano kati ya sita katika familia ya mhubiri Bw Boniface Opetuh na Bi Monica Aloo.

Alilelewa katika utamaduni uliosisitiza ulazima wa mtoto kuadhibiwa na kushauriwa na mzazi yeyote kwa kuwa jukumu la ulezi lilikuwa la jamii nzima. Ingawa hivyo, mapitio hayo magumu katika maisha ya utotoni hayakumtamausha wala kumvunja moyo.

Alitazamia kwamba siku moja angeweza kuyaboresha mazingira ya jamii yake, aishi kwa staha na uadilifu wa kiwango cha juu ili awe kielelezo kwa wengi.

Opetuh alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Lukongo alikosomea kati ya 1992 na 2001. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliotia fora zaidi katika mtihani wa KCPE 2001, hususan katika somo la Kiswahili.

Alama nzuri alizozipata mtihanini zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya Musanda, Mumias mwanzoni mwa 2002. Akiwa huko, alikuwa kati ya wanafunzi waliostahiwa pakubwa na walimu wao kwa hulka nyerezi na taadhima tele. Mbali na uigizaji, alishiriki michezo ainati kama vile kabumbu, pete na voliboli. Hizi ni fani na sanaa zilizoanda kujikuza ndani ya Opetuh tangu akiwa mtoto mdogo.

Aliufanya mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2005 na akafaulu vyema. Ufanisi huo ulimwezesha kujiunga na Chuo cha Walimu cha Tambach, eneo la Kerio (Iten), Kaunti ya Elgeyo Marakwet mnamo 2007.

Alipokuwa Tambach, alipata mwamko mpya wa kukizamia Kiswahili kwa mapana na kukipigia chapuo kwa ari na idili. Alichangia kishujaa ufufuzi na uendeshaji wa Chama cha Kiswahili katika Chuo cha Walimu cha Tambach kilichowahi kumwaminia kuwa mwenyekiti. Alifuzu mnamo Machi 2010 baada ya kuhitimu na kukamilisha mtihani wake wa PTE mnamo Septemba 2009.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kusomea shahada katika taaluma ya ualimu (Kiswahili na Historia.) Anatazamia kuhitimu mwakani majaliwa.

Opetuh anatambua upekee wa mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza vilivyo, kumshauri ipasavyo, kumhangaikia kwa kila hali na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali. Mbali na wazazi, mwingine aliyemshajiisha zaidi kujitahidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili Bi Fatuma Kombo.

Anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa na kuhamasishwa pakubwa na mwalimu huyu.

“Nilivutiwa mno na lafudhi ya Bi Kombo, nikatamani sana ije siku ambapo nami ningekuwa na umilisi mkubwa wa lugha, nikisarifu Kiswahili kama yeye.”

Akiamini kwamba kinolewacho hupata na ukiona vyaelea vimeundwa, Opetuh alijitolea kwa udi kujifunza Kiswahili na kukitetea vilivyo. Utashi wake katika lugha hii ulikua na kupevuka kiasi kwamba wengi aliosoma nao walipania sana kumuiga.

Kariha na ilhamu zaidi ya kukichangamkia Kiswahili ilichangiwa na wanafunzi wenzake waliovutiwa mno na ufasaha wake kila alipoyatema maneno ya lahaja mbalimbali za Kiswahili. Ari yake ya kutaka Kiswahili kipate makao salama na ya kudumu moyoni mwake iliamshwa na mwalimu wake wa shule ya upili Bi Belinda Omuholo. Huyu alitangamana naye kwa karibu sana, akampokeza malezi bora zaidi ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichapukia Kiswahili alaa kulihali.

Zaidi ya Bi Omuholo aliyemtanguliza vyema katika somo la Fasihi ya Kiswahili, mwingine aliyemchochea pakubwa kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi; ni Bw Gichiko aliyemfundisha katika Chuo cha Walimu cha Tambach.

Ualimu

Tangu ajitose kikamilifu katika ulingo wa ualimu mnamo 2010, Opetuh amefundisha Kiswahili katika shule mbalimbali jijini Nairobi. Alihudumu katika Shule ya Msingi ya Hope Academy (mtaa wa Fedha) kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuhamia Twin-Star Academy (mtaa wa Imara Daima) alikoamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Tangu 2012, Opetuh amekuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika shule ya msingi inayomilikiwa na Kanisa la Pentecostal Fellowship of Africa (PEFA) katika mtaa wa Donholm.

Uzoefu anaojivunia katika ufundishaji, utahini na usahihishaji wa mitihani ya kila sampuli umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa

kwa mitihani ya kitaifa. Zaidi ya kuandaa na kuhudhuria makongamano mbalimbali katika jitihada za kuchangia makuzi ya Kiswahili, amewahi pia kualikwa kufundisha, kuwashauri na kuwaelekeza walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali za msingi ndani na nje ya Kaunti ya Nairobi.

Anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayempokeza elimu na maarifa. Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni PEFA Donholm ni nguzo ya mafanikio yao mitihanini.

Baadhi ya walimu hao ni Vincent Kimwele, Stephen Nalami, Sharon Nyakundi, Lydia Oloo, Winnie Muthini, Lydia Omagwa, Michael Otieno, Dorcas Vaati na Eric Andati (Mwalimu Mkuu).

Zaidi ya kuwashirikisha wanafunzi wake katika tamasha za kitaifa za muziki na drama, pia amekuwa akiwakuza vilivyo katika utunzi wa mashairi, uigiza na michezo ya kandanda, voliboli na kuteleza kwa viatu vya chuma (skating).

Jivunio

Mbali na kuwa katika Jopo la Walimu ambalo hutungia kampuni ya Signal Printers, Nairobi mitihani ya somo la Kiswahili, Opetuh amekuwa mshauri na mhariri wa baadhi za hadithi za watoto na machapisho mbalimbali katika kampuni ya Moran (EA) Ltd. ‘Sarufi Kwa Shule za Msingi’ ni kitabu cha hivi karibuni ambacho ameihariria Moran.

Ndoto ya uandishi ilianza kumnyemelea tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Nyingi za insha bora alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno.

Waliomhimiza pakubwa kwa kuiwasha moto azma yake katika ulingo wa utunzi wa kazi za kibunifu ni aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa PEFA Donholm, marehemu Samuel Mbau, Samuel Ng’ang’a (Moran Publishers), Francis Nziya (Signal Publishers), Timothy Sumba Omusikoyo (mwandishi wa Moran na Signal Printers) na Stephen Oluoch ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Tassia Catholic School, Nairobi.

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu, Opetuh pia amelivalia njuga suala la ufugaji na ukuzaji wa mimea mbalimbali. Anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili. Kwa pamoja na mkewe Bi Sheila, wamejaliwa mtoto mmoja wa kiume, Teddy Cruz.