TAHARIRI: Mitihani: Wasimamizi waachane na uzembe
Na MHARIRI
MTIHANI wa Darasa la Nane (KCPE) unapomalizika leo, mambo mengi yamejitokeza ambayo kama taifa, hatuna budi kuketi chini na kuyatathmini.
Mbali na visa vya mimba za mapema ambavyo hata mwaka jana nchi nzima ilipiga kelele kuvihusu, yapo masuala yanayohusiana na mustakbali wa siku za usoni za jamii nzima.
Japokuwa kwa kiwango kikubwa, serikali ilikuwa imejiandaa vyema kuhakikisha kuwa mtihani huu unamalizika bila kuwepo visa vingi vya udanganyifu, ilifeli katika kuthibitisha kuwa wanafunzi walisajiliwa ipasavyo.
Kwa mfano katika Kaunti ya Kakamega, ilifichuka kwamba wanafunzi wa shule ya umma walisajiliwa kama watahiniwa wa kibinafsi.
Huu huenda ulikuwa uzembe kwa upande wa Mwalimu Mkuu, lakini pia wizara ya Elimu ilikuwa na jukumu la kufuatilia kwa makini kujua kama kweli kila mtoto aliye katika darasa la nane amesajiliwa kufanya mtihani.
Labda pengine siku za usoni, Bunge lapaswa kubuni sheria ya kuwalazimisha wakuu wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kuwatumia wazazi maelezo kamili kuhusu usajili wa watoto wao katika mitihani.
Wala hatutakuwa tunakiuka sheria yoyote. Shughuli kama za uchaguzi, huwashirikisha watu kukagua madaftari ya wapigakura, ili kuangalia kama maelezo kuwahusu yapo sahihi. Isitoshe, wapigakura wanaposajiliwa hupewa kadi maalum iliyo na maelezo hayo.
Hili likifanywa kwa watahiniwa, itakuwa rahisi kwa wazazi, walimu na maafisa wa wizara ya Elimu kuwa na maelezo sahihi kuwahusu watahiniwa. Kuketi na kusubiri hadi siku ya mtihani na kuanza kugutuka kuwa eti mwanafunzi hajasajiliwa, ni uzembe unaoweza kuepukwa.
Kubwa zaidi kwenye mtihani huu, ni taarifa kuwa wanafunzi 11 katika kaunti ya Tharaka Nithi hawajafanya mtihani huo, baada ya wazazi wao kujiunga na madhehebu ya Kabonokia.
Kundi hili limekuwa likitumia vibaya kifungu cha 32(4) cha Katiba kwamba “Mtu hatalazimishwa kufanya, kujihusisha na kitendo chochote kilicho kinyume na dini au Imani yake.”
Kuwaondoa watoto shuleni kwa kisingizio kuwa Kabonokia hawaamini katika kuenda shuleni, ni kinyume na sera ya serikali ya kuwapatia watoto wote elimu bila malipo. Wazazi wa watoto hao yafaa wasakwe, wakamatwe.