KILIMO NA BIASHARA MASHINANI: Shule iliyo mstari wa mbele kufunza wanafunzi kilimo kukabili baa la njaa
Na SAMMY LUTTA
SHULE ya Msingi ya Pokotom mjini Kakuma, Kaunti Ndogo ya Turkana Magharibi ina idadi ya wanafunzi 1,500.
Wanafunzi wengi wanonekana wakikimbia kwenye mabweni ili watoe sare za shule na kuvalia nguo za michezo ili kucheza kandanda, voliboli, mbio na michezo mingine.
Tunavutiwa na watoto 60 ambao wanajihusisha na ukulima wa kumwagia mashamba maji karibu kwenye shamba lao ambalo liko nyuma ya jikoni ya shule.
Wengi wao hawana haja ya kwenda kwa mabweni kwanza kwa sababu lazima wamwagie mimea ya mboga tofauti tofauti maji baada ya jua kali la linaloshuhudiwa kila mara eneo hilo.
Kipande cha shamba cha Nicholas Naokot, 17, wa Darasa la Sita kina kunde za siku 20 na mchicha. Pamoja na miti mia moja ambayo alipanda na mwenzake Jonathan Umoja, anatarajia kupata faida ya Sh2,500 kwa kuuza mazao kwa wiki.
Naokot anaeleza kuwa aliamua kujiunga na kilabu cha wakulima mwaka jana ili kumsaidia mamake Esther Lokopon ambaye hana kazi na anategemea chakula cha msaada.
“Tangu nianze ukulima, shamba hili limekuwa likinisaidia sana kwa sababu kando na kuuza mboga, huwa nachuna kila mara na kupelelekea mama ili aandae chakula nitakachokula pamoja na ndugu wangu sita,” alielezea huku akingo’a magugu ya nyasi kwenye shamba.
Alisema kuwa nyumbani ni kijiji cha Highlands, kilomita 15 kutoka shuleni na kuna mawe mengi ambayo yamefanya iwe changamoto kwake kuanzisha mradi wa ukulima ili awafunze wadogo zake.
Naokot alisema kuwa awali chakula alichokuwa akikipata nyumbani ni mahindi na maharagwe na mwalimu wa ukulima Sarah Terigen alikuwa akisisitiza kuwa lishe bora lazima iwe na matunda na mboga za majani.
“Kwa sasa kila nikifika nyumbani na mboga na nipate kila mtu ametabasamu, hali hiyo inanipa moyo wa kutia bidii na kufuata kila maelezo ninayopewa na mwalimu wangu, Bi Terigen,” aliongezea.
Shule hiyo iko na wanafunzi wa kutoka jamii ya Turkana na wengine kutoka Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma na kupitia kwa ukulima wanatangamana na kujifunza mengi.
Maji mengi ambayo yanatumika kwa shamba hilo yanaelekezwa kutoka jikoni pindi baada ya kutumika kuosha vyombo na kwa mifereji ambayo wanafunzi hutumia kunawa mikono.
Mwalimu Terigen alisema kuwa alipata mafunzo kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linalofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ili kuhakikisha wanafunzi shuleni humo wanajihusisha na ukulima.
“Nilianzisha mradi huo wa chakula 2018 baada ya kufunzwa na Shirika la FAO na nahamasisha walimu wenzangu, wanafunzi na wazazi kukumbatia ukulima. Shule imetuchangia pakubwa kwa sababu inanunua mboga aina ya kunde na malenge kutoka mashamba yetu,” alisema.
Mapato wanayopata kwa pamoja wanatumia kiasi kununulia wanafunzi wasiojiweza sare za shule na vitabu baada ya kuhakikisha wako na mbegu na madawa ya wadudu.
Kando na shamba wako na mradi wa kufuga kuku wa kienyeji ambapo kando na wanafunzi kujifunza pia, tayari kuku 30 wametolewa ili wajifunze ufugaji huo na kupata mayai na nyama.
Wadudu waharibifu
Alisema kuwa wangependa kufanya ukulima wa sukumawiki lakini wadudu hushambulia kila mara wanapopanda.
“Tunataka tuongeze shamba ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi wa Darasa la Sita kwenda chini wamekumbatia ukulima. Lengo letu kuu ni kukabiliana na njaa kupitia ukulima unaoendeshwa na wanafunzi,” Terigen alisema.
Shule hiyo iko na shamba la mafunzo alafu baadaye wanafunzi wanasonga kwa shamba lingine ambapo wanagawiwa sehemu ya kupanda vyakula wanavyotaka.
Kando na maji ambayo wanapata kutoka kwa mifereji na jikoni shuleni, kila kunaponyesha wanafunzi hupumzika kunyunyuzia mashamba maji na pia kuhakikisha wanavuna maji ya mvua.
Afisa wa FAO Kaunti ya Turkana Daniel Irura alisema kuwa wakazi wengi pamoja na Shule eneo hilo wanakosa lishe bora kwa vile wengi hutegemea mboga kutoka Kitale ambayo iko kilomita 450.
“Shirika la FAO linashirikiana na serikali ya Kaunti ya Turkana ili kuhamasisha wakazi pamoja na Shule kuanzisha mashamba madogo ya kupanda mboga huku wakitumia maji ambayo wanamwaga baada ya kuosha vyombo na shughuli zingine za nyumbani,” alisema Irura.