Nyuki wasababisha watahiniwa wa kiume kufanyia mtihani katika shule ya wasichana
NA KALUME KAZUNGU
WATAHINIWA 50 wa mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) walijeruhiwa Jumatano bumba la nyuki lilipoanguka ghafla katika uwanja wa shule ya msingi ya wavulana ya Lamu.
Nyuki hao baadaye walitawanyika kwa haraka madarasani na kuwashambulia watahiniwa na wasimamizi wa mtihani huo.
Kisa hicho kilitokea saa nane na robo, muda mfupi baada ya watahiniwa kuanza mtihani wao wa somo la uandishi wa Insha.
Aidha ilikuwa mguu niponye kwa kila mtu aliyekuwa kwenye uwanja wa shule hiyo, ikiwemo maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda kituo hicho cha mtihani, ambapo walikamata bunduki zao na kufyatuka mbio kutoroka makali ya nyuki hao waliokuwa wengi ajabu.
Shughuli za mtihani kwa zaidi ya watahiniwa 100 wa KCPE pamoja na wengine zaidi ya 10 ambao ni watahiniwa binafsi shuleni humo zilisitishwa kwa zaidi ya dakika 20.
Wasimamizi wa mtihani huo walilazimika kuwahamisha watahiniwa hao wavulana kutoka shuleni mwao hadi katika shule jirani ya msingi ya wasichana ya Lamu ambako baadaye waliruhusiwa kuendelea na kukamilisha uandishi insha.
Katika mahojiano na Taifa Leo, mmoja wa wasimamizi wakuu wa KCPE kituoni humo ambaye alitaka tusichapishe jina lake alieleza kustaajabishwa kwake na mkasa huo.
“Tulishangaa kuona nyuki wakitushambulia ghafla kutoka kila mahali. Mimi mwenyewe ndiye niliyeathirika zaidi kwa kuumwa na nyuki hao pindi walipoanguka kama jiwe kwenye uwanja wa shule, karibu na mahali nilipoketi. Nimeumwa kichwa, macho, mikono, mashavu na miguu. Nahisi uchungu kila mahali,” akasema afisa huyo.
Mmoja wa watahiniwa binafsi shuleni humo, Bw Omar Anafolly alisema uvamizi wa nyuki hao ulisababisha wanafunzi wengi kuchanganyikiwa wasijue la kufanya.
Bw Anafolly alitaja uvamizi wa nyuki hao kwa watahiniwa wa KCPE wa Lamu kuwa “ni mazingaombwe.”
“Hii haikuwa hali ya kawaida. Kila mmoja wetu amechanganyikiwa kabisa lakini tunashukuru kwamba licha ya majeraha tuliyopata kwa kuumwa na wadudu hao hatari, hakuna hata mmoja wetu amefariki. Pia tunaishukuru serikali kwa kuchukua hatua za haraka kutuhamisha hadi shule ya wasichana ambako tuliendelea na kumaliza mtihani wetu,” akasema Bw Anafolly.
Baadhi ya wanafunzi aidha walipelekwa hospitalini kufuatia majeraha mabaya waliyopata kwa kuumwa na nyuki hao.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia amethibitisha tukio hilo na kusema ni mwanafunzi mmoja ambaye alipata majeraha mabaya.
“Ni kweli. Kumekuwa na uvamizi wa nyuki kwenye shule ya wavulana ya Lamu. Wanafunzi walikuwa wakiendelea na mtihani wao wa KCPE. Mwanafunzi mmoja alijeruhiwa vibaya na kulazwa kwenye hospitali ya King Fahad mjini Lamu. Wanafunzi wamehamishwa hadi kituo kingine ili kuendelea na mtihani wao. Juhudi za kuwaondoa nyuki zinaendelea na tunatumai hali itakuwa shwari shuleni humo wakati wowote. Watu wasiwe na shaka,” akasema Bw Macharia.