Habari Mseto

Raia wa Amerika aliyejeruhi koplo sasa yuko huru

October 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Amerika aliyemchapa na kumuumiza afisa wa polisi katika hoteli ya Azuri jijini Nairobi amesamehewa na kuachiliwa huru.

“Nimemsamehe Alex Harpe aliyenipiga na kunijeruhi. Amenilipa fidia ya Sh200,000. Sitaki kuendelea na kesi hii. Nimemsamehe,” Koplo Duncan Kiprono amemweleza hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bi Hellen Onkwani jana.

Akiongozwa kutoa ushahidi mbele ya hakimu na kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka, Koplo Kiprono ameeleza mahakama kwamba walifanya mashauri na mawakili wa mshtakiwa na kuafikiana alipwe fidia ya Sh200,000.

“Tuliafikiana na mawakili wa mshtakiwa kwamba nilipwe fidia kisha nitamatishe kesi hii,” amesema mlalamishi huyo.

Koplo Kiprono amesema chini ya sheria za kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani, ameona heri amsamehe mshtakiwa na kisha “atamatishe kesi.”

“Je, unajua ukiondoa kesi hii hutairudisha tena hapa mahakamani?” Bw Gachoka amemwuliza Koplo Kiprono.

“Ndio; ninajua hayo barabara,” amejibu mlalamishi.

Mahakama imetamatisha kesi hiyo na kumwachilia mshtakiwa huyo kwa dhamana katika shtaka lingine la kuzua fujo na kuhatarisha amani katika hoteli ya kifahari ya Azuri.

Mshtakiwa alikuwa amekana kwamba alisababisha fujo kwa kumfukuza afisa anayepokea wageni mle hotelini.

Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili kwa maagizo zaidi.

Mshtakiwa alikana kwamba alizua vurugu mnamo Oktoba 14, 2019.

Aliposhtakiwa wiki iliyopita, mshukiwa huyo, mahakama iliagiza azuiliwe katika gereza la Viwandani kwa siku sita.