• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
MBURU: Serikali isihadae kuhusu uchumi, Wakenya wanaumia

MBURU: Serikali isihadae kuhusu uchumi, Wakenya wanaumia

Na PETER MBURU

SERIKALI kudai kuwa uchumi wa taifa unazidi kukua wakati mamilioni ya Wakenya wanazidi kulia kutokana na ugumu wa maisha ni kinaya kikubwa na ishara ya jinsi tuko katika kile tunachoweza kusema ni ‘Kenya mbili’.

Hii ni kwa kuwa licha ya kudai kuwa mambo yako sawa kiuchumi, idadi ya watu ambao wamefutwa kazi baada ya waajiri wao kushindwa kuhimili ugumu wa kiuchumi inazidi kuongezeka kwa maelfu, huku kampuni zaidi zikiendelea kutangaza mipango ya kufuta wafanyakazi.

Mitaani na vijijini, Wakenya wanateseka kwa kukosa kazi, mapato madogo kwa walio na kazi na mfumkobei wa bidhaa muhimu, hasa vyakula.

Tafiti za kiuchumi miaka ya majuzi zimeonyesha jinsi Wakenya wamekuwa wakikopa bidhaa za kimsingi kama vyakula madukani ili kuendesha maisha, kando na wengine wengi ambao wanazidi kufilisika na kuuza mali, ama kufunganya virago na kurudi mashambani kutoka mijini, kutokana na kulemewa na gharama ya maisha.

Maelfu ya wanafunzi wanazidi kufuzu kutoka vyuo, lakini wanaishia kukaa manyumbani kutokana na ukosefu wa kazi, wakati nyingi za kazi zilizopo serikalini zinapewa wazee wakongwe.

Ndiposa, pamoja na Wakenya wengi, tunashindwa kuelewa ni uchumi gani ambao serikali inazungumzia inaposema kuwa Kenya inazidi kukua, kwani hatuhisi chochote.

Ni kinaya kikubwa ikiwa uchumi unaimarika machoni pa serikali, lakini kwa wananchi unazidi kuzorota.

Unapodurusu mitandaoni ama kuzungumza na watu, ishara zote ni wazi kuwa Wakenya, haswa vijana, wana hasira- wamekasirikia serikali na viongozi kwa kuwatelekeza na kuwafanya kuadhibiwa vikali na uchumi.

Kitu cha pekee ambacho serikali imekuwa na bidii ya kuwapa Wakenya, hata bila kuitishwa- ni ahadi, ahadi kuwa kilimo kitaimarishwa, afya na elimu kuboreshwa, vijana kupewa kazi na kila Mkenya kuhakikishiwa anapata chakula.

Lakini kwa bahati mbaya, nyingi za ahadi hizi zimesalia kuwa hivyo tu, nyoyo na mawazo ya Wakenya yakishibishwa matarajio, lakini uhalisia wa maisha ukiwa kinyume kabisa.

Serikali yenyewe huongoza juhudi za kuwapelekea Wakenya wanaoishi kaskazini mwa nchi na maeneo mengine yanayokumbwa na mafuriko ama kiangazi misaada ya vyakula na vitu vingine vya kimsingi, ishara wazi kuwa bado kuna tatizo.

Ripoti za uchumi kukua haziwezi kuwa na maana yoyote kwa Wakenya ambao hali ya maisha inazidi kuharibika.

You can share this post!

TAHARIRI: Wizara ihakikishe kila mtoto anapata elimu

Uhuru ana mwaka hajaenda ‘nyumbani’

adminleo