Habari

Oparanya akashifu wakaguzi wa vitabu vya fedha

November 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya amewashutumu baadhi ya wakaguzi wa vitabu vya fedha dhidi ya kuitisha hongo ili kutoa huduma fulani.

Akizungumza wakati wa kikao cha kujadiliana kati ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na CoG kuhusu kuzuia ufisadi mnamo Alhamisi katika hoteli ya Naivasha, alisema baadhi ya mashirika yanapaswa kupigwa msasa.

Alidai kuwa ana ushahidi wa maovu yanayoendelezwa na wakaguzi wa vitabu vya fedha akitaja suala hilo kama changamoto katika vita dhidi ya ufisadi kwenye vitengo vya ugatuzi.

“Tumeshuhudia visa ambapo wakaguzi wa vitabu vya fedha wameitisha rushwa ili kutoa huduma maalum, tuna ushahidi,” alisema Bw Oparanya. Gavana huyo wa Kakamega alitoa wito kwa EACC kuchunguza taasisi kama hizo akisema kumekuwa na ukiukaji wa michakato ya usimamizi wa fedha katika viwango vyote viwili vya serikali.

Alizungumza kuhusu mahusiano yenye chuki kati ya serikali hizo mbili akisema hali hiyo ilikuwa imezua ufa unaowezesha ufisadi kunawiri. Aidha, alikashifu baadhi ya mashirika ya kibinafsi ikiwemo wanakandarasi na wauzaji bidhaa akisema kunao waliokuwa wakiendesha ufisadi kwenye kaunti.

“Ili kupigana vilivyo na ufisadi tunapaswa kuangazia kikamilifu uovu huo,” alisema mwenyekiti wa COG.

Alifichua kuwa vita dhidi ya ufisadi wakati mwingine vilionekana kuwa vigumu kutokana na watu walio mamlakani wanaonufaika kutokana na uhalifu huo.

“Vita dhidi ya ufisadi vinazidi kuwa vigumu kwa sababu kuna watu uongozini ambao wameamua kunufaika kutokana na mifumo iliyopo na viongozi hawana nia wala uwezo wa kuwakomesha kufanya hivyo,” alisema.