Maafisa zaidi ya 20 wakamatwa, wengine kadha wasakwa na polisi kuhusu vyeti
Na MWANDISHI WETU
AFISI ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) imewakamata maafisa na watu zaidi ya 20 kutoka Idara ya Usajili wa Umma (DCR) na kuanzisha msako mkali dhidi ya wengine kadha kuhusiana na madai ya ufisadi katika usajili wa vyeti vya kuzaliwa.
Maafisa hao kutoka idara mbalimbali za taasisi hiyo wanashutumiwa dhidi ya kutengeneza vyeti ghushi kwa raia wasio wa Kenya pamoja na kuitisha hongo kutoka kwa umma.
Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai jana alitoa orodha ya maafisa hao 24 wanaoandamwa akisema operesheni hiyo itaendelezwa katika hospitali kadha Nairobi zinazoaminika kuwa sehemu ya mashirika yanayoendeleza uhalifu huo.
“Afisi za serikali si maficho ya mawakala na wahalifu kujitajirisha kwa kutapeli umma,” alisema.
Miongoni mwa wanaosakwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Kimaeneo CRB Paul Kagiri, Afisa Mkuu wa kuweka Rekodi Charles Akwoni, Afisa Mkuu wa Usajili wa Umma Charity Mwadime pamoja na msaidizi wake Bi Jane Maina.
Wengine ni pamoja na maafisa wa usajili wa umma Bw Patrick Silla na Bw Peter Nganga, maafisa wasaidizi Bi Joyce Keitany, na Bw Maxmilla Ouma.
Haya yamejiri siku chache tu baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Katibu Karanja Kibicho kupiga kambi katika afisi za CRB, Upper Hill, Nairobi ambapo waliapa kuendelea kufanya hivyo hadi mabadiliko yote yaliyopangiwa kufanyika katika utowaji wa vyeti vya kuzaliwa na vya kifo, yatakapotekelezwa.
“Tumekuwa hapa tangu wiki jana ikiwemo wikendi ili kujibu kilio cha Wakenya kuhusiana na ucheleweshwaji wa kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa,” alisema Bw Matiang’i ambaye pamoja na Bw Kibicho wamekuwa wakizuru idara hiyo kila siku kuanzia Ijumaa wiki iliyopita.
Hatua hiyo ambayo haikutarajiwa ilitokana na kilio cha raia kuhusiana na kujikokota kwa mchakato wa utowaji wa nakala hizo katika Afisi za ACK Bishop House.
Maafisa wakuu wawili wa CRB walisimamishwa kazi ambapo uchunguzi kuhusiana na madai hayo unaendelea.
“Ufisadi hauna nafasi Serikalini na katika Wizara ya Usalama wa Ndani. Tutakabiliana nao vilivyo. Ukiona mawakala wowote nje ya majengo haya, wanapaswa kukamatwa mara moja,” alifoka Matiang’i.