• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
DAU LA MAISHA: Anafinyanga vijana kitabia na kabumbu

DAU LA MAISHA: Anafinyanga vijana kitabia na kabumbu

Na PAULINE ONGAJI

ANATUMIA soka kuwapa matumaini watoto wanaoishi katika mazingira ambapo kuna changamoto ya kujiendeleza kutokana na ugumu wa maisha.

Kutana na Beldine Odemba, 35, mkufunzi mkuu na kocha wa klabu ya soka ya Kariobangi Sharks, mtaani Kariobangi, jijini Nairobi.

Amefuzu na ana leseni ya kiwango C na hati ya ukufunzi wa soka mashinani huku mchango wake ukitikisa sio tu mtaa huu, bali pia umevutia jicho la wadau wa soka kimataifa.

Aidha ni mmoja wa wakufunzi kadha kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni wanaowania taji la WorldRemit Future Stars.

Katika kinyang’anyiro hiki, Bi Odemba ambaye mbali na kuwa kocha wa soka, pia amesomea masuala ya uchapishaji wa kieletroniki chuoni, atatoana kijasho na makocha wengine wa kike na kiume, humu nchini na kimataifa.

Endapo atashinda taji hili, basi atapata fursa ya kufanya mazoezi pamoja na makocha wa klabu ya Uingereza ya Arsenal.

“Kama kocha wa kukuza vipaji, huo utakuwa ufanisi mkubwa hasa ikizingatiwa kwamba Arsenal ni klabu kubwa na maarufu duniani. Hii itanipa uzoefu na elimu zaidi ya soka,” asema.

Hata hivyo anasisitiza kwamba endapo atashinda, ufahamu atakaopata utakuwa na mchango mkubwa katika jamii. “Kupitia ujuzi huu, soka mtaani Kariobangi na nchini kote itabadilika kabisa,” aongeza.

Aliwezaje kupaa na kufikia kiwango cha kutambulika kimataifa? Katika kazi yake ya ukufunzi, Bi Odemba anatoa mafunzo kwa timu tano katika klabu ya Kariobangi Sharks.

“Mimi ni mkufunzi mkuu wa timu ya wavulana wasiozidi miaka 10 na 15. Aidha, mimi ni kocha msaidizi wa timu ya wavulana wasiozidi miaka 13 na 17. Pia, mimi ni mkufunzi msaidizi wa timu ya wasichana wasiozidi miaka 16 ya Kariobangi Sports,” aeleza.

Huu ukiwa mwaka wake wa 20 tangu ajitose katika ukufunzi, anajivunia mataji mbalimbali nchini na nje. “Tumeshinda mataji kadhaa humu nchini, lakini upeo ulikuwa mwaka jana tulipomaliza nafasi ya pili katika kombe la East Africa Cup 2018 kwa timu ya soka kwa wavulana wasiozidi miaka 13,” asema.

Mbali na kutoa mafunzo ya soka, jukumu lake pia linahusisha kufinyanga tabia miongoni mwa watoto huku akitoa huduma zake kwa watoto wavulana na wasichana.

“Kama kocha wa timu tano, matamanio yangu ni kuona wachezaji wangu wakiendelea kuimarika nje na ndani ya uwanja. Nia yangu sio tu kuimarisha vipaji vyao kama wanasoka, bali pia kuchangia vyema maishani mwao kwa kuwakuza vyema kitabia,” aeleza.

Ukocha

Safari ya Bi Odemba kama kocha ilianza mwaka wa 1999 kupitia shirika la Mathare Youth Sports Association (MYSA) huku ari yake ikichochewa na ndugu zake waliomhimiza kuwarai wasichana zaidi kujihusisha na kabumbu.

“Nilipoanza hakukuwa na wasichana katika timu yangu mtaani Dandora ambapo nililazimika kucheza miongoni mwa wavulana,” aeleza.

Kama mkufunzi mtaani Kariobangi, anasema kwamba mambo hayajakuwa rahisi kwani changamoto ni nyingi.

“Mwanzoni changamoto kuu ilikuwa kudunishwa hasa kwa sababu za kijinsia. Lakini nina furaha kusema kwamba sikuwaruhusu waliokuwa na nia ya kutumia jinsia yangu kunidhalilisha kufanikiwa katika njama zao,” aeleza.

Pia, anazungumzia changamoto ya ukosefu wa fedha, suala linalosababisha ukosefu vifaa vya mazoezi vilevile uwanja wa kufanyia mazoezi.

“Aidha, watoto wengi ninaowashughulikia wanatoka katika familia maskini, na ni changamoto kuwakuza katika pande zote, kimaadili na hata uwanjani,” asema.

Lakini hayo kamwe hayajazima kiu yake ya kutumia mchezo huu kuhakikisha kwamba bali na kukuza vipaji vya soka, mtaa wa Kariobangi pia unatambulika kama chimbuko la wataalamu wa nyanja zingine, vilevile wananchi waadilifu.

You can share this post!

Mashahidi 68 kuitwa katika kesi inayomkabili Waititu

Sonko atolewa pumzi

adminleo