• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
Maafisa zaidi ya 20 katika sakata ya vyeti kufikishwa kortini

Maafisa zaidi ya 20 katika sakata ya vyeti kufikishwa kortini

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA zaidi 20 wa Idara ya Usajili wa Watu ambao walikamatwa Ijumaa kwa kushiriki ufisadi katika utoaji vyeti vya kuzaliwa na vya vifo katika makao makuu ya idara hiyo Jumatatu watafikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka.

Maafisa hao, ambao wanajumuisha mameneja wa idara mbalimbali katika ofisi hizo zilizoko jumba la Bishop House, Nairobi walikamatwa Ijumaa katika operesheni ambayo imesababisha hofu katika ofisi za idara hiyo kote nchini ambako uovu huo umekithiri.

Miongoni mwa waliokamatwa ni naibu mkurugenzi wa idara hiyo Paul Kagiri, meneja wa kitengo cha usimamizi wa rekodi Charles Akwoni, Charity Mwandime (afisa mkuu wa usajili wa watu), manaibu wake Jane Wangari na Daniel Ngamba na makarani kadhaa.

Walizuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi wakihojiwa.

Wapelelezi walisema Kagiri na wenzake pia wamekuwa wakiendeleza kashfa ya kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wageni, wakisaidiana na wahusika fulani katika hospitali binafsi ambao hughushi kadi za kuzaliwa.

Kadi hizo bandia ndizo wao hutumia kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wateja wao.

Hii ndiyo maana miongoni mwa waliokamatwa, ni wafanyakazi wanne wa Hospitali ya St Francis iliyoko eneo la Kasarani, Nairobi huku wengine wakidaiwa kutoroka kuepuka kukamatwa.

Shughuli sambamba

Polisi wanaamini kuwa Kagiri na Akwoni ndio wahusika wakuu katika sakata hiyo kwani wanaendesha shughuli sambamba za utoaji vyeti katika mojawapo ya makazi yao jijini Nairobi.

Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kufika ghafla katika ofisi za idara hiyo ambapo alishuhudia mwenyewe mahangaiko ambayo Wakenya hupitia wakitafuta stakabadhi hizo muhimu.

Inadaiwa kuwa matapeli wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa idara ya usajili wa watu katika jumba hilo – Bishop House – kuitisha ada za “kuharakisha” utoaji stakabadhi hizo kutoka kwa watu ambao huwatafutia watoto wao.

Mnamo Ijumaa, Dkt Matiang’i akiandamana na mwenzake wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru, walizuru ofisi za Bishop House na kukashifu mtindo wa maafisa wa serikali kugeuza utoaji wa huduma za serikali kuwa njia ya kujitajirisha kwa kuitisha hongo.

“Kile kimejitokeza hapa ni kwamba wafanyakazi wa serikali wanawanyima wananchi huduma ili waweze kutoa stakabadhi hizo kwa wageni walioingia nchini kinyume cha sheria,” Dkt Matiang’i akasema.

Akasisitiza: “Hatutavumilia yale tunayoyashuhudia hapa ambapo watu wanakuja asubuhi (kusaka vyeti vya kuzaliwa) na wanaondoka jioni bila stakabadhi hizo huku watu wengine wakipata kwa njia ya mkato.”

You can share this post!

Kilimohai chapigiwa chapuo

Mechi saba wikendi hii ligi ya daraja la pili

adminleo