Liverpool itabomoa Aston Villa – Owen
Na MASHIRIKA
MERSEYSIDE, Uingereza
ALIYEKUWA mshambuliaji matata wa kitaifa, Michael Owen amesisitiza kwamba Liverpool ina uwezo mkubwa wa kuicharaza Aston Villa zitakapokutana leo Jumamosi alasiri ugani Villa Park.
Liverpool wataingia uwanjani kujaribu kuhifadhi uongozi wao wa mwanya wa pointi sita kileleni, mbele ya Manchester City ambao watakaokutana nao Novemba 10.
Vijana hao wa Jurgen Klopp waliandikisha ushindi wa 2-1 majuzi dhidi ya Tottenham Hotspur kutokana Jordan Henderson na Mohamed Salah, lakini kwa taabu.
Liverpool inajivunia rekodi ya kushinda mechi 10 za ligi kuu, hata baada ya kucheza na Arsenal, Chelsea na Manchester United pamoja na Spurs.
Lakini leo watakuwa wakicheza dhidi ya Aston Villa ambao pia wameanza msimu huu vizuri katika mechi zao 10 za kwanza tangu warejee ligini.
Villa walishindwa 3-0 na Manchester City ugani Etihad juma lililopita, hali inayomfanya Owen kuamimi watalazwa na Liverpool.
“Niliposhuhudia wakicheza na Manchester City, niliona udhaifu wao na sioni wakifanya chochote mbele ya Liverpool,” alisema.
“Dhidi ya Brighton walishambuliwa mara 20, sababu inayonifanya niipe Liverpool nafasi kubwa ya kushinda mechi ya leo,” aliongeza.
Ripoti ya daktari
Katika mechi ya leo Jumamosi, kocha Dean Smith anasubiri ripoti ya daktari kuhusu hali ya nahodha Jack Grealish aliyekosa mechi ya katikati mwa wiki dhidi ya Wolves katika pambano la Carabao Cup.
Wakati huo huo, klabu ya Roma wako tayari kuwapa Manchester United Sh1.6 bilioni kumnunua Chris Smalling baada ya beki huyo kuvuma tangu ajiunge na klabu hiyo ya Serie A kwa mkopo.
Muingereza huyo mwenye umri wa miaka 29 alijiunga na Roma mwezi Agosti kwa msimu mmoja baada ya kiwango chake kudaiwa kushuka, lakini ameshangaza kwa kujumuishwa kikosini na kocha Paulo Fonseca tangu wakati huo, akifunga bao lake la kwanza majuzi katika ushindi wao wa 4-0 dhidi ya Udinese, Jumatano usiku.
Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza ameichezea Manchester United tangu 2010 na angali na mkataba na klabu hiyo ya EPL hadi 2022.
Roma imefurahishwa na uchezaji wake na wako tayari kumnunua wakati wowote. Habari za hivi karibuni zimesema kwamba Roma inajiandaa kutoa kiasi cha Sh1.8 kwa ajili ya kumsajili beki huyo matata.
Tayari klabu hiyo ya Serie A imewalipa Manchester United Sh360 milioni kwa muda atakapokuwa Roma kwa mkopo msimu huu.
Roma wako tayari kumpa beki huyo mkataba wa miaka mitano na sasa wanasubiri kuona iwapo Manchester watakubali ofa hiyo.
Smalling aliondoka baada ya Harry Maguire na Victor Lindelöf kutua Old Trafford katika kikosi ambacho pia kinajivunia uwepo wa Marcos Rojo na Phil Jones kama mabeki wa katikati.