Kiunjuri atosha kuwa msemaji Mlima Kenya – wabunge
Na GEORGE MUNENE na WANDERI KAMAU
BAADHI ya wabunge wa chama cha Jubilee, wanamtaka Waziri wa Kilimo Bw Mwangi Kiunjuri kuwa msemaji wa kisiasa eneo la Mlima Kenya pindi Rais Uhuru Kenyatta ataondoka uongozini jinsi inavyotarajiwa ifikapo mwaka 2022.
Wabunge Kabinga Thayu (Mwea), Munene Wambugu (Kirinyaga ya Kati) na Zachary Thuku (Kinangop) walimtaja Bw Kiunjuri kama mwanasiasa mwenye tajriba kubwa ambaye ana uwezo wa kuwaunganisha viongozi wote katika eneo hilo.
Wakihutubu katika Shule ya Msingi ya Nyakiungu, Kaunti ya Kirinyaga mnamo Ijumaa, wabunge hao walimwambia Bw Kiunjuri kuchukua uongozi mara tu baada ya Rais Kenyatta kuondoka uongozini.
“Bw Kiunjuri ni mwanasiasa mwenye tajriba kubwa. Hivyo, anapaswa kuteuliwa kuwa msemaji mkuu wa eneo hilo. Tunamtaka atuongoze na kutueleza mwelekeo wa kisiasa tutakaochukua,” akasema Bw Thuku.
Wabunge hao walisema watawashinikiza wenzao kumuunga mkono Bw Kiunjuri kuchukua nafasi hiyo.
Walisisitiza kuwa eneo hilo linahitaji wanasiasa wenye uwezo mkubwa kama Bw Kiunjuri ili kupigania maslahi ya wakazi.
“Tunahisi kuwa eneo hili linapaswa kutengewa fedha zaidi kwani linachangia pakubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa kitaifa. Ni Bw Kiunjuri pekee ambaye ana uwezo kuhakikisha kuwa tumepata mgao ufaao wa kifedha,” akaongeza Bw Wambugu.
Naye Bw Thayu alimsifu waziri huyo kama kiongozi mwenye bidii, anayepaswa kuungwa mkono kama kiongozi mkuu wa kisiasa wa eneo hilo.
Madiwani watano kutoka Bunge la Kaunti ya Kirinyaga pia waliunga mkono kauli ya wabunge hao.
Madiwani hao wanajumuisha Pius Njogu kutoka wadi ya Thiba, Bw Gudson Muchina (Tebere), Bw Erastus Ireri ( Ngariama), Friendrick Bundi (Njukiini) na Bw Kinyua Wangui wa wadi ya Mutira.
Bw Kiunjuri kwa upande wake aliwaomba viongozi kuungana ili kupigania eneo hilo kuongezwa mgao wa kifedha.
“Ikiwa viongozi wataendeleza mgawanyiko, basi eneo hili litabaki nyuma kimaendeleo,” akaongeza.
Masilahi ya wakulima
Kauli hiyo inajiri wakati Bw Kiunjuri ameendelea kukosolewa pakubwa kwa madai ya kutotetea masilahi ya wakulima.
Wakulima kutoka eneo hilo wamekuwa wakilalamika kuhusu kudorora kwa sekta ya kilimo, hasa mazao muhimu kama majanichai, kahawa, pareto, mpunga na miraa kwani ndiyo kitegauchumi cha wakazi wengi.
Hata hivyo, Bw Kiunjuri amejitetea vikali, akisema kuwa usimamizi mbaya wa vyama vya ushirika vinavyosimamia uuzaji wa mazao hayo ndivyo vimechangia kudorora kwa mapato wanayopata wakulima.
Bw Kiunjuri anahusishwa na kundi la ‘Tangatanga’ ambalo limekuwa likimpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022.
Kando na Bw Kiunjuri, viongozi wengine ambao wamependekezwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ni magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Kiraitu Murungi (Meru), Mwangi wa Iria (Murang’a), Francis Kimemia (Nyandarua), wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a) kati ya wengine.
Hata hivyo, Rais Kenyatta amejitenga na midahalo ya urithi wa kisiasa, akisisitiza kuwa wananchi ndiyo wataamua kuhusu watakaowaongoza.