'Yanayowakuta wajane yasiwafishe moyo kusukuma gurudumu la maisha'
Na SAMMY WAWERU
KATIKA jamii nyingi Barani Afrika, kumesikika visa vingi ambapo mume pindi anapofariki, jamaa zake huhangaisha mke mjane kwa kumnyang’anya mali aliyoachiwa kurithi.
Jambo la kufisha moyo zaidi ni pale mume na mke walikuwa wametafuta mali pamoja.
Hizo ni dhuluma ambazo hapa nchini Kenya hushuhudiwa mara kwa mara.
Endapo wazazi wa mume kuanzia awali walipinga uhalali wa ndoa ya mwana wao, maji huzidi unga anapoaga dunia na kuacha mke na watoto.
Pia, hali huwa si hali tena ikiwa bwana hakuwa ameacha urathi – kauli aitoayo mtu kupitia maandishi, juu ya umiliki wa mali yake kabla ya kufariki. Kisa cha Susan Wangui, ambaye ni msanii wa nyimbo za injili na mfanyabiashara, ni mojawapo ya vingi ambavyo wanawake wajane hupitia.
Masaibu yake yalianza pindi tu mume wake alipofariki 2012, urithi wa shamba ukiwa ndicho kiini kikuu.
Mjane huyo ambaye ni mama wa watoto wawili, alijitosa katika usanii kupitia nyimbo alizotunga kujifariji.
Ni hatua ambayo imegeuka kuwa ni kitega uchumi, na kila anapopata fursa kutumbuiza kwa nyimbo zake anajizolea umaarufu.
“Kwa mwezi sikosi baina ya hafla mbili hadi nne, kila moja nikitoza wastani wa Sh5,000,” anadokeza Bi Susan ambaye ana umri wa miaka 28.
Isitoshe, kwa mwezi huuza zaidi ya kanda 150, moja ikigharimu Sh200. Ni msanii wa nyimbo za injili na ameziimba kwa lugha ya Agikuyu, Swahili na Kiingereza.
Ana albamu mbili; ‘Akeneri Uuru’ (wanaofurahia maovu) na ‘Muti wa Mugaa’ (mti wa Januari), kila moja ikiwa na nyimbo sita. Mbali na mialiko, hutumia mitandao ya kijamii kama vile You-tube, Instagram, Facebook na Whats App kuvumisha nyimbo zake.
Kulingana na Dianah Kamande, mjane na mwasisi wa shirika la kutetea haki za wajane na mayatima nchini, ‘Cometogether Widows and Orphans Organization’, Susan anapaswa kutambua kuwa yeye sasa ndiye ‘mama na baba’ ya watoto alioachiwa.
Nafasi ya mwanamke katika jamii
Akitilia mkazo nafasi ya mwanamke katika jamii, Bi Kamande anamhimiza kukaza kamba kupalilia kipaji alichotunukiwa na Mungu, uimbaji.
“Unyanyapaa na vita dhidi ya wajane na mayatima ni mambo yanayofanyika nchini. Muhimu ni kukubali umeachwa mjane, utafutie watoto riziki kwa njia ifaayo kama vile kuwekeza katika biashara,” anaeleza kiongozi huyo ambaye mwaka 2018 alipokea tuzo ya HSC na inayotolewa na Rais kwa Wakenya waliojitolea kuimarisha jamii kwa hali na mali.
Dianah Kamande anafafanua kwamba haja ipo wajane kujiunga na makundi au mashirika ya kijamii yanayotetea haki zao pamoja na za watoto yatima.
“Kwa mfano, shirika nililoanzisha huimarisha kina mama wajane kifedha na kuhakikisha mayatima wanasoma na kupata elimu bora,” anasema.
Kupitia hilo, Dianah anasema kwa msanii kama Susan atapata wateja watakaonunua kanda zake na hata wafadhili wanaoinua mashirika hayo.
Mwanamuziki huyo kutoka Kaunti ya Nyeri pia ni mfanyabiashara, anayeshona vitambaa vya sofaseti, makateni (curtains) na mapazia. Mjasirimali huyo anasema kuwa biashara hiyo imesaidia kufanikisha usanii wake.