DINI: Endapo ya jana ni ya kukutamausha, usitazame nyuma
Na FAUSTIN KAMUGISHA
MATENDO bila dira ni kupitisha muda tu. Dira bila matendo ni ndoto za mchana, lakini dira pamoja na matendo vinaweza kubadili dunia, aliwahi kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini marehemu Nelson Mandela.
Ukiwa unaelewa unapoelekea na kama dira ni nzuri, hakuna kutazama nyuma.
Tunasoma hivi katika Injili “Mtu aliyetia mkono wake kulima kwa plau akitazama nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu” (Luka 9:62).
Mtakatifu Augustini alisema: “Ni kama alisema Mashariki ikikuita usitazame Magharibi.”
Kama ya jana ni ya kukatisha tamaa, usitazame nyuma. Kama yaliyopita ni ukongwa la utumwa (Gal 4: 31b-5:1, 13-18) usitazame nyuma. Kama yaliyopita yanakufanya uwe na chuki usitazame nyuma. Kama yaliyopita hayakuleti karibu na Mungu, usitazame nyuma.
Kama matendo yako ya jana unayaona kama takataka, usitazame nyuma. Kama yaliyopita ni mazuri lakini ni adui wa mazuri zaidi ya yajayo usitazame nyuma.
Kuzitazama mara nyingi tabia mbaya tulizoziacha nyuma kunaweza kuturudisha huko. Eliya alihakikisha lile la kumfanya atazame nyuma amewagawia watu (1 Fal. 19: 16b. 19-21).
Neno uaminifu katika maisha ya ndoa ni gumu kulisema. Ni gumu kulitaja lakini ni gumu zaidi kuliishi. Kwa vyovyote, maji ukiisha yavulia nguo, huna budi kuyaoga.
Usitazame nyuma. Wengine baada ya kukaa na mwenzi wa ndoa wanagundua walifanya makosa.
Mwanaume aliyeoa alimuuliza padri: Ulihubiri Jumapili asubuhi kuwa ni jambo baya watu kujipatia faida kutokana na makosa ya wengine. Unakubaliana na hilo padri?” Padri akamjibu: “Hiyo ni sheria ya Mungu.”
Mtu huyo aliendelea: “Kwa mantiki hiyo, unaweza kunirudishia elfu ishirini nilizokupa kwa kutufungisha pingu za ndoa miaka mitano iliyopita. Nilifanya makosa na wewe umefaidi makosa yangu.”
Nyuma kukiwa kweusi mbele ya Yesu huwa ni kweupe. Matumaini yanakwambia ingawa nyuma ni kweusi mbele ni kweupe. Mbele hulea lakini nyuma hailei.
Ni methali ya Kiswahili. “Unaweza kulala chini na kufa, au unaweza kusimama na kupigana, lakini hilo sawa hakuna kurudi nyuma,” alisema Jon English.
Kaza nia kwenda mbele kabla ya kukata tamaa. Mtazame Yesu vipingamizi na vizingiti alivyovuka na upinzani aliokutana nao. Hata hivyo alikaza nia ya kwenda mbele.
“Kabla ya kukata tamaa, tazama nyuma na kusoma masuto yaliyosemwa dhidi ya Lincoln,” alisema Bruce Barton aliyekuwa mbunge wa Amerika (1886-1967).
“Tazama zawadi iliyoko mbele, usirudi nyuma,” alisema Bill Clinton Rais wa 42 wa Amerika (1993-2001), aliyezaliwa 1946.
Shivaji Mkuu (1630-1680) alikuwa ni mfalme wa Maratha. Alikuwa na vita na mfalme Mughal Aurangazeb mara nyingi. Kuna wakati alishiriki mapambano amesimama juu ya dimbwi. Shivaji na askari wake walipanda kwa msaada wa kamba.
Akihisi kuwa wanaelekea kushindwa, Dadaji, kapteni wa jeshi la Shivaji alianza kuteremka akitumia kamba. Shivaji alikata kamba ili jeshi lake lisikwepe vita.
Amri kwa kapteni
Alitoa amri kwa kapteni wa jeshi lake: “Badala ya kurudi nyuma kuwa na ujasiri na kupigana.” Dadaji alipata nguvu mpya na ujasiri alianza kupigana tena. Hatimaye Aurangazeb alishindwa.
Kama haujapotea njia, hakuna kurudi nyuma bali kuendelea mbele. Kwa kumfuata Yesu Kristo haujapotea njia hakuna kurudi nyuma.
“Haijalishi umeenda umbali kiasi gani; kama umepotea njia, rudi nyuma,” ni methali ya Kituruki.
Rudi nyuma iwapo umepotea. Lakini kama haujapotea hakuna kurudi nyuma.
Mtakatifu Thomas Kempis anatuasa. “Mngonje Bwana. Tenda kiungwana, na kuwa na ujasiri. Kuwa na imani, lakini kaa mahali pako na usirudi nyuma,” alisema Thomas wa Kempis.
Kama nyuma umevuruga panakatisha tamaa usitazame nyuma.