Marufuku ya plastiki yamchochea Criticos kuwekeza upya kwa mikonge
BRIAN OCHARO na CHARLES WASONGA
MWEKEZAJI Basil Criticos anafufua kilimo cha mkonge kilichosambaratika zaidi ya mwongo mmoja uliopita ili kufaidi kutokana na hatua ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.
Mkulima huyo ambaye ni Mbunge wa zamani wa Taveta, amewekeza mamilioni ya fedha katika kilimo cha mkonge kilichofifia serikali ilipotwaa ekari 15,000 za shamba lake mnamo 2008 ambako alikuwa akikuza mmea huo.
Anasema anatumani kwamba biashara yake itavuma tena sasa ambapo kuna hitaji kubwa la makonge nchini na katika mataifa ya Afrika Mashariki.
Hapa nchini makonge yanahitajika kwa wingi kama malighafi ya kutengeneza mifuko ya kubebea bidhaa.
Bw Criticos sasa anatarajia kuvuna mmea huo alioupanda mnamo 2012 katika shamba lake la ukubwa wa ekari 500.
“Kwa kuwa mifuko ya plastiki imepigwa marufuku nchini kwa kusababisha uchafuzi wa mazingira, naamini kuwa hitaji la makonge litapanda zaidi,” akasema.
Serikali ya kitaifa ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Agosti 28 mwaka 2017.
Miadi
Bw Criticos anasema kufikia sasa amepata miadi kutoka kwa wateja wengi ambao wangetaka kununua makonge yake miezi 12 kabla ya kuvuna.
“Hitaji ni iko juu zaidi… lakini kwa kuwa bei ya makonge hupanda kila mara sitaki kuwapa wateja ahadi ya kuwauzia wakati huu.
“Kuwekeana miadi na wateja nyakati zingine huwa sio nzuri kwa sababu wanunuzi hao watakufunga kiasi kwamba hautaweza kuwauzia wengine ambao watakuwa tayari kununua kwa bei ya juu,” mkulima huyo wa asili ya Ugiriki akaeleza.
Kabla ya kuporomoka kwa sekta ya makonge mnamo 2008, Bw Criticos alinawiri katika kazi hiyo kiasi kwamba aliwezi kuanzisha maghala makubwa ya makongo katika miji ya Kitui, Homa Bay na Kendu Bay.
Kupokonywa ardhi
Mkulima huyo anasema utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki ulimpokonya ardhi licha ya kukubali kulipa deni la Sh55 milioni la benki moja kwa awamu.
Bw Criticos anasema baada ya kilimo cha mkonge kuporomoka, zaidi ya wafanyakazi wake 1,200 walipoteza ajira.
“Lakini nashukuru Mungu nimerejea katika biashara tena, kujikokota kutoka hasara kama hiyo siyo haijakuwa jambo rahisi.,” akasema.
Bw Criticos anasema anapanga kuongeza shamba lake la mkonge kutoka ekari 500 za sasa hadi ekari 800 katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Wakati huu, ameajiri zaidi ya wafanyakazi 100.
Humu nchini Mkulima huyo huuza zao lake kwa kampuni ya East African and Cordage ambayo hununua makonge kwa wingi.
Meneja mkuu wa kampuni hiyo James Maka alisema makonge hutumiwa kutengeneza nguo na karatasi. Mmea uliokomaa unaweza kuwavunwa kwa zaidi ya miaka mitano.
Kando na hayo, miti ya makonge hutumiwa kama kuni ya kupikia na kujengea nyumba, haswa katika fuo za bahari.
Ukuzaji na utunzaji wa mmea wa mkonge ni wa gharama ya chini ikilinganishwa na mimea mingine inayohitaji mvua nyingi, kuwekwa mbolea na unyunyiziaji wa dawa za kuangamiza wadudu waharibifu.
Makonge hutumiwa kutengeneza kamba, karatasi, nguo, viatu, kofia, mifuko, msala, bodi za kuchezea mchezo wa vishale huku mabaki yakitumiwa kutengeneza mbolea.