• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
WASONGA: Kibra wapuuze Raila, Ruto wajichagulie kiongozi bora

WASONGA: Kibra wapuuze Raila, Ruto wajichagulie kiongozi bora

Na CHARLES WASONGA

UCHAGUZI mdogo katika eneobunge la Kibra umegeuka kuwa wa aina yake kutokana na sababu kwamba wanasiasa vigogo wameugeuza kuwa uwanja wa kujipima nguvu kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Inaudhi kwamba Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wametumia muda wao mwingi sio kuvumisha uwezo na sifa za wagombeaji wa vyao bali ni kujipiga vifua, kila mmoja akielezea namna atamfunza mwenzake adabu.

Kwa mfano, katika msimu wa kampeni, unaokamilika leo, Dkt Ruto amekuwa akiwaambia wafuasi wa Jubilee kwamba ushindi wa mgombeaji wa chama hicho MacDonald Mariga utaashiria “ushindi wetu huko mbele.” Hapa humaanisha ushindi wake katika uchaguzi mkuu ujao.

Naye Bw Odinga amenasibisha eneobunge la Kibra na chumba chake kulala huku akisema kushindwa kwa mgombeaji wa ODM Benard Okoth Imran, itakuwa aibu kubwa kwake.

“Msiniabishe kwa kupigia watu wengine kura. Kura kwa Imran ni sawa na kura kwangu,” Bw Odinga amekuwa akisema kila mara.

Kwa mtazamo wangu, kauli kama hizi ni kauli za kuwapotosha wapigakura kusudi wasifanye maamuzi yao Alhamisi wiki hii.

Ukweli ni kwamba wapigakura 118,000 katika eneo la Kibra watafika debeni kuchagua mmoja kati ya wagombeaji 24 ambao wanashindania kiti hicho kilichosalia wazi baada ya kifo cha Ken Okoth mnamo Julai 26 mwaka huu.

Kati ya wagombeaji hao ni pamoja na Mariga, Imran, Eliud Owalo (wa ANC), Khamisi Butichi (Ford Kenya) na wengineo wala sio Ruto, Raila Mudavadi au Moses Wetang’ula.

Nawaomba wakazi wapuuze porojo za wanasiasa hawa wakuu na watumie busara ya kiwango cha juu wanapofanya uamuzi utakaoamua mustakabali wao katika kipindi cha mitatu iliyosalia kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao.

Wanafaa wachague yule ambaye wameshawishika kuwa ana uwezo na moyo wa kuendeleza kazi nzuri ambayo ilitekelezwa na marehemu Okoth katika kipindi cha miaka saba ambacho alihudumu kama mbunge wa Kibra.

Wasifanye uamuzi huo kwa misingi ya vyama, ukabila na dini. Na wasichague mgombeaji fulani kwa sababu aliwahonga kwa pesa nyingi wakati wa kampeni wakifanya hivyo watajuta wenyewe baadaye.

Eneobunge la Kibra, zamani likiitwa Lang’ata, linakumbwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, uhaba wa umeme na maji, ukosefu wa vyoo bora na barabara nzuri katika vitongoji mbalimbali huku idadi kubwa ya wakazi wakizongwa na umasikini.

Isitoshe, eneo hili ndilo lina mtaa mkubwa wa mabanda nchini na wa pili barani Afrika.

Ndio maana eneo hili linahitaji mbunge mwenye maono, aliye na ufahamu wa changamoto hizi pamoja na mikakati faafu ya kuzikabili. Kibra inahitaji kiongozi mwenye ujuzi katika nyanja ya usimamizi na anayeweza kuwasilisha matatizo yanayowakumba wakazi bungeni na katika asasi nyinginezo za serikali.

Hii ni kwa sababu kando na utungaji sheria na uhakiki wa utendakazi wa serikali kuu, wajibu mwingine mkuu wa mbunge ni uwakilishi.

You can share this post!

Mwanamume mwenye bashasha amuua mkewe

OBARA: Miundomsingi mijini izingatie uboreshaji afya ya...

adminleo