• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Je, Kibra watachagua sera au umaarufu?

Je, Kibra watachagua sera au umaarufu?

Na BENSON MATHEKA

Huku kampeni za uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra zikiingia kipindi cha lala salama, wapigakura wataamua iwapo watamchagua mbunge kwa sababu ya sera na ahadi zake au umaarufu wa chama chake.

Wadadisi wa siasa wanasema, wagombeaji wanne wakuu katika uchaguzi huo unaolenga kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Ken Okoth wamekuwa wakitoa ahadi nyingi kuwarai wapigakura, baadhi ambazo haziwezi kutimilika.

“Ukweli ni kwamba uchaguzi huo unahusu masuala mawili- umaarufu wa vyama vya kisiasa na wagombeaji wenyewe na sera na ahadi wanazowapa wapigakura kwenye kampeni.

“Hata hivyo, kama ilivyo wakati wa kampeni za uchaguzi, ahadi za baadhi ya wanasiasa huwa ni mlima kutekeleza au hazitekelezeki kabisa. Huwa za kuwavutia wapigakura tu,” aeleza mdadisi wa siasa Karanja Kamau.

Wagombeaji wakuu katika uchaguzi huo ni Eliud Owallo wa chama cha Amani National Congress (ANC), Benard Okoth Imran wa chama cha ODM, Khamisi Butichi wa chama cha Ford Kenya na Macdonald Mariga wa chama cha Jubilee.

Bw Mariga ambaye umaarufu wake unatokana na chama cha Jubilee, kuungwa mkono na Naibu Rais William Ruto na baadhi ya wabunge wa chama hicho amekuwa akivutia halaiki kwenye mikutano yake ya kampeni.

Hata hivyo, wadadisi wanasema japo amekuwa akilenga vijana kwenye ahadi anazotoa, nyingi zinaweza kuwa hewa tupu. “ Atakayechaguliwa kuwa mbunge wa Kibra atahudumu kwa miaka miwili na nusu na kuna ahadi ambazo wagombeaji wamekuwa wakitoa za kufurahisha wapigakura tu,” asema.

Miongoni mwa ahadi ambazo Bw Mariga amekuwa akitoa ni kuhakikisha vijana wa Kibra watatengewa nafasi maalumu wakati wa usajili wa makurutu wa vikosi vya usalama, jambo ambalo wadadisi wanasema kisheria haliwezekani, kuhakikisha wakazi wote wanafaidika na basari za elimu ilhali zinatengewa wasio na uwezo na kuzindua vituo vya mafunzo ya kazi katika eneo hilo.

Wadadisi wanasema kuwa matamshi ya viongozi wanaompigia debe Bw Mariga ambaye tiketi yake kwenye uchaguzi huo iligawanya zaidi chama cha Jubilee, yanaweza kumkosesha kura nyingi.

“Inashangaza viongozi wanaomuunga mkono kama Naibu Rais William Ruto wanaweza kuwaambia wapigakura wa Kibra kwamba watapata maendeleo kutoka kwa serikali tu wakimchagua Mariga kama mbunge wao.

“Hivi ni vitisho kutoka kwa kiongozi wa serikali vya kutenga watu ambao wana haki ya kupata maendeleo licha ya mrengo wa siasa wanaoegemea,” alisema.

Bw Mariga pia ameahidi wakazi kuwa wakimchagua kuwa mbunge wao, atashirikiana na wizara ya fedha ili iweze kuwapa mikopo wafanyabiashara wadogo wadogo ilhali wizara hiyo haitoi mikopo kwa watu binafsi.

Wadadisi wanasema japo Bw Okoth anategemea umaarufu wa chama cha ODM na kuungwa mkono na baadhi ya wabunge wa chama cha Jubilee, kauli mbiu yake ya “Elimu bora”, “Mazingira bora” na “Uchumi bora” inaweza kuwachangamsha wapigakura pia.

Akiwa alihudumu kama mwenyekiti wa kamati ya hazina ya eneobunge la Kibra marehemu Ken Okoth alipokuwa mbunge wa eneo hilo, Imran anafahamu vyema matatizo ya elimu ya wakazi ambayo yalimfanya mtangulizi wake kuwa maarufu.

Ameahidi kuwa atazindua mpango wa kunufaisha wafanyabiashara kupitia maonyesho ya bidhaa za Jua Kali ili kusaidia wafanyabiashara kupata masoko na wateja.

Hata hivyo, wadadisi wanasema ahadi hii inaweza kuwa hewa tu kwa sababu hakueleza atakavyowasaidia wapigakura kuanzisha na kukuza biashara zao.

“Alikuwa katika kamati ya CDF na mshirika wa karibu wa ndugu yake Ken Okoth, mbona hakumshauri kuanzisha miradi hii anayodai ataanzisha katika kipindi cha chini ya miaka miwili atakayokuwa mbunge iwapo atashinda.

“Mbona hakumshauri au kuanzisha miradi ya kuimarisha mazingira katika mtaa wa Kibra akiwa mwenyekiti wa CDF? Ahadi za wagombeaji hawa ni feki,” alisema Bw Athumani Ali, mkazi wa eneo la Lindi mtaani Kibra.

Wadadisi wanasema Bw Owalo, ambaye alihama ODM muda mfupi kabla ya kiti cha eneobunge la Kibra kutangazwa wazi, amekuwa akiendesha siasa zake wa ukomavu kwa kuwatembelea wapigakura waliko na kuwauzia sera zake chini ya kauli mbiu yake ya Liwe Liwalo na Owalo.

Wadadisi wanasema azima ya Owalo kutaka kuwakilisha Kibra bungeni, haikuanza baada ya kifo cha Ken Okoth.

“Amejisawiri kama mtu anayeelewa na kuhisi shida wanazopitia wakazi wa Kibra eneo ambalo sawa na Imran alizaliwa. Alianza kusaidia wakazi hata kabla ya kiti hicho kuwa wazi. Anaelewa vyema wanachohitaji wakazi wa Kibra kwa sababu alikuwa mpanga mikakati wa kampeni za kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga,” asema mdadisi wa siasa Ben Mogaka.

Bw Odinga amewahi kuwa mbunge wa eneo hilo.

Bw Owalo ambaye amekuwa akipigiwa debe na kiongozi wa chama cha ODM amedumisha lugha ya heshima katika kampeni za kuuza sera zake ambako ameahidi vijana kuwa njia ya pekee kukabiliana na ukosefu wa ajira ni kupitia mafunzo. Aidha, ameahidi kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, makazi na michezo.

“Nafikiri kuna kitu ambacho wapigakura wa Kibra watakosa wakikosa kumchagua Owalo. Kampeni zake zimekuwa zikihusu sera zake kwa Kibra na sio kujipiga kifua au kuzua ghasia,” alisema Bw Mogaka na kuongeza huwa huenda hii ndiyo sababu wapinzani wake hushambulia misafara yake ya kampeni.

Mgombeaji wa chama cha Ford Kenya, Khamisi Butichi naye amekuwa akiahidi kuimarisha huduma za wakazi wa Kibra, kuhakikisha watoto wamepata elimu bila ubaguzi.

Butichi anasema anaelewa matatizo ya wakazi wa Kibra kwa kuwa alizaliwa eneo hilo.

You can share this post!

OBARA: Miundomsingi mijini izingatie uboreshaji afya ya...

SHANGAZI: Mpenzi anarusha chambo kisiri kwa rafiki yangu

adminleo