Michezo

KRU kuchunguza madai ya dhuluma za kimapenzi dhidi ya msanii

April 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA
KWA mara ya kwanza Chama cha Raga Nchini (KRU) kimezungumzia madai ya ubakaji yanayowakabili wachezaji wawili wa raga.

Wawili hao mwishoni mwa juma walishutumiwa na mwanamuziki mmoja kwa jina Wendy Kemunto kwa kumbaka mnamo Februari mwaka huu.

Kwenye taarifa kupitia tovuti yake, KRU, Jumatatu ilisema itashughulikia suala hilo kulingana na sera zake.

“Chama cha Raga Nchini (KRU) kimefahamisha kuhusu ripoti inayohusu madai ya dhuluma za kimapenzi yaliyowahusisha wachezaji wa timu ya Kenya ya wachezaji Saba kila Upande.

Suala hilo litachunguzwa haraka iwezekanavyo na KRU, kulingana na kanuni zinazoongoza wachezaji waliopewa kandarasi,” ikasema taarifa hiyo.

Pia ni muhimu kutambua kwa walinda usalama wamepashwa habari kuhusu madai hayo na KRU haiwezi kutoa maelezo zaidi kuhusu madai hayo hadi uchunguzi utakapokamilika na matokeo yake kutolewa rasmi.

“Hata hivyo, KRU ingependa kueleza kuwa hairuhusu visa vya dhulumu za kimapenzi au vitendo vyovyote vinavyokiuka Kanuni zilizowekwa na Chama cha Raga Duniani. Chama hiki kimejitolea kuendelea kuheshimu, kutoa nafasi na kuwawezesha wanawake kushirikishwa katika fani zote za mchezo wa raga,” taarifa hiyo ilisema.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) inasema kuwa inachukulia madai hayo kwa uzito mkubwa na kwamba imezungumza na msanii huyo aliyedai kudhulumiwa na wachezaji hao.